Tuesday, April 14, 2015

WAMILIKI WA MABASI WAELEZA SABABU ZA AJALI BARABARANI.




Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kimesema kutosimamiwa vizuri kwa ratiba za mabasi za kuondoka eneo moja kwenda lingine, ni miongoni mwa mambo yanayochangia ajali za barabarani kutokana na madereva kukimbizana.

Kauli hiyo ya Taboa imekuja siku moja baada ya basi la Nganga Express lililokuwa likitokea Kilombero kwenda Mbeya kugongana na lori aina ya Fusso, kisha magari hayo kushika moto na kusababisha vifo vya watu 18.

Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu alisema jana kuwa: “Mfano hai yapo mabasi yanakwenda kwa kasi kutoka Dar es salaam hadi karibu na Same mkoani Kilimanjaro ndiyo yanasimama porini ili kusubiri muda ufike,” alisema.

“Ratiba ile inaonyesha kwamba ukitoka Ubungo saa fulani unatakiwa kufika kituo B au C saa fulani. Sasa mabasi haya yanawahi tena wakati mwingine saa mbili nzima...yanapita wapi? alihoji.

Alisema ajali nyingine zimekuwa zikisababishwa na makosa ya kibinadamu ya madereva.
“Sisi tunasisitiza udereva uwe taaluma, tuachane na madereva wanaopita magari mengine barabarani hata katika maeneo yasiyoruhusiwa,” alisema Mrutu.

Hata hivyo, alitaja tatizo lingine kuwa ni miundombinu mibovu ya barabara, akisema zina mashimo katikati na nyingine nyembamba.

Wakati huohuo, Chama cha Wasafirishaji Abiria (Akiboa), mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara wamewatupia lawama askari wa usalama barabarani.

Mwenyekiti wa Akiboa, Hussein Mrindoko aliwalaumu askari hao kusahau kukagua malori na magari madogo ambayo nayo ni kiini cha ajali. Mrindoko alisema mzigo mkubwa wanabebeshwa madereva wa mabasi tu.

Hata hivyo, Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Johansen Kahatano alisema kuhusu madai ya baadhi ya askari kutosimamia ratiba atachunguza.

Mmiliki wa mabasi ya Ngorika, George Temba alisema ratiba ya mabasi zaidi ya 20 kuondoka muda mmoja ni tatizo.

0 Responses to “WAMILIKI WA MABASI WAELEZA SABABU ZA AJALI BARABARANI.”

Post a Comment

More to Read