Wednesday, May 13, 2015
WILAYA YA MBEYA MJINI YAONGOZA KWA MATOKEO BORA YA KUJIFUNZA
Do you like this story?
13 Mei 2015, Dar es Salaam: Watoto wa Afrika
Mashariki hawajifunzi stadi za msingi za kusoma na kuhesabu. Ni watoto wawili
tu kati ya kumi (20%) wa darasa la tatu wanaoweza kusoma na kufanya hesabu za
darasa la pili. Wanapohtimu elimu ya msingi, mtoto mmoja kati ya wanne Afrika
Mashariki (24%) anakuwa bado hajamudu stadi za kusoma na kuhesabu.
Matokeo haya yametolewa na Uwezo iliyopo
Twaweza, kwenye ripoti yao Je, Watoto wetu wanajifunza? Uwezo wa kusoma na
kuhesabu Afrika Mashariki. Takwimu za matokeo ya kujifunza, hali ya shule na
kaya zilikusanywa mwaka 2013. Zilijumuisha wilaya zote Afrika Mashariki kupitia
tathmini ya kaya iliyofanywa na wananchi wenyewe. Matokeo ya kujifunza
hutathminiwa kwa watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 16 kupitia majaribio
yaliyotungwa kwa mtaala wa ngazi ya darasa la pili.
Asilimia 64 ya watoto Kenya walifaulu
majaribio yote ya kusoma na kuhesabu. Nchini Tanzania ni asilimia 48 na Uganda
asilimia 36 tu waliofaulu majaribio yote. Hii ina maana kwamba, hata Kenya, nchi
inayofanya vizuri kuliko zote Afrika Mashariki, ina watoto asilimia 36
wasiozimudu stadi za msingi za kusoma na kuhesabu katika ngazi ya darasa la
pili.
Wilaya ya Mbeya Mjini imeibuka kuwa wilaya
yenye ufaulu wa juu kabisa Afrika Mashariki. Hata hivyo, wilaya nyingine kumi
zenye ufaulu wa juu zimetoka nchini Kenya. Wilaya za Tanzania mara nyingi
hupata ufaulu wa kati wakati Uganda imekuwa ilishika nafasi ya chini kabisa.
Wilaya iliyofanya vizuri zaidi nchini Uganda ilishika nafasi ya 82 kati ya
wilaya zote za Afrika Mashariki.
Kipato cha familia kimeonekana kuwa na
uhusiano na matokeo ya kujifunza: lipo pengo kubwa kati ya maskini na wasio
maskini
Asilimia 70 ya watoto nchini Kenya waliotoka
kaya zisizo maskini walifaulu jaribio moja la kusoma na kuhesabu. Ni asilimia
44 tu ya watoto waliotoka kaya maskini sana waliokuwa na uwezo huo huo.Asilimia
55 ya watoto nchini Tanzania waliotoka kaya zisizo maskini waliofaulu jaribio
moja la kusoma na kuhesabu. Ni asilimia 39 tu ya watoto waliotoka kaya maskini
sana waliokuwa na uwezo huo huo.Asilimia 42 ya watoto nchini Uganda waliotoka
kaya zisizo maskini waliofaulu jaribio moja la kusoma na kuhesabu. Ni asilimia
24 tu ya watotowaliotoka kaya maskini sana waliokuwa na uwezo huo huo.
Licha ya tofauti zilizopo nchini Kenya, kaya
maskini zaidi nchini humo, bado zinafanya vizuri kuliko kaya zisizo maskini za
Uganda.
Cha kusikitisha ni kuwa hakuna mabadiliko
makubwa kwenye matokeo ya kujifunza kwa kipindi cha miaka minne iliyopita (2010
hadi 2013). Licha ya uandikishaji umebaki kuwa juu tangu kuanzishwa kwa elimu
ya bure ya msingi kwa wote katika nchi zote tatu.
Vipimo vya Uwezo hutumiwa kutathmini mwenendo
wa utekelezaji wa Malengo ya Elimu kwa Wote. Malengo haya yaliahidiwa
kutekelezwa ndani ya kipindi cha miaka 15 kuanzia 2000 hadi 2015 na yalilenga
kuinua ubora wa elimu. Kwa ujumla, hakuna mabadiliko makubwa kwenye kiashiria
chochote kilichotumika kutathmini malengo haya ndani kipindi cha miaka minne
iliyopita. Hata hivyo, uandikishaji umebaki kuwa juu katika nchi zote tatu
zikiwa na wastani wa uandikishaji wa 90%. Vile vile usawa wa kijinsia umefikiwa
katika nchi zote tatu kwenye nyanja za uandikishaji na ubora. Hakuna tofauti
iliyobainika kwenye fursa ya kuandikishwa kati ya wavulana na wasichana.
Lakini, usawa huo huo upo pia kati ya wavulana na wasichana katika kufanya
vibaya kwenye matokeo ya kujifunza.
Dk. John Mugo, Mkurugenzi wa Utafiti wa
Twaweza alisema "tofauti kubwa baina ya nchi na baina ya wilaya,
zinaonesha kuwa Afrika Mashariki itaendelea kugawanyika zaidi. Aidha, utafiti
huu unaonyesha kwamba matokeo hayajabadlika miaka yote hii. Hii hi ishara tosha
kwamba hatujatilia mkazo umuhimu wa watoto wote kujifunza wakiwa shuleni"
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa
Twaweza, aliongeza "Mafanikio yaliyofikiwa katika kuongeza fursa za
kujiunga na shule na usawa wa kijinsia yanapaswa kupongezwa. Lakini takwimu
hazifichi ukweli kwamba wananfunzi wengi mno baado hawajifunzi. Tusilegeze uzi
katika uandikishaji wa watoto. Jambo la msingi zaidi ni kuhakikisha kwamba watoto
wote wananjifunza stadi zote za msingi – kusoma na kuhesabu."
Uwezo ilitathmini watoto zaidi ya 325,000
wenye umri kati ya miaka 6-16 katika takriban kaya 150,000. Hii ilijumuisha
wilaya 366 nchini za Kenya, Tanzania na Uganda. Pia ilikusanya takwimu kutoka
shule za msingi za serikali zaidi ya 10,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WILAYA YA MBEYA MJINI YAONGOZA KWA MATOKEO BORA YA KUJIFUNZA ”
Post a Comment