Friday, November 20, 2015
MAMBO MATATU KWA WENYE WAPENZI WACHUNAJI.
Do you like this story?
Huko mtaani ambapo imekuwa ni kitu cha
kawaida kumsikia msichana akitamba mbele za wasichana wenzake kwa kusema; ‘Mimi
nina pedeshee wangu bwana, kila ninachotaka ananipa, anajua asiponipa namtosa
tu, yaani namchuna kama sina akili nzuri.’
Si hivyo tu, wapo wanaume pia ambao ni kero
kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za
kutegemea kupewa kila kitu na wapenzi wao hata kama wanao uwezo wa kuvipata
vitu hivyo kama watajishughulisha.
Unaweza kumsikia mwanaume akisema; ‘Aaah!
Yule demu kazimika ile mbaya na mapigo yangu, kila ninachotaka ananipa, anajua
akinizingua namtosa, hadi mshahara wake akipata ananigawia.’
Ninachotaka kusema leo ni kwamba, mapenzi ya
kweli hayana uhusiano wowote na pesa, ukiona mpenzi wako anaweka pesa mbele na
ukishindwa kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini,
hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.
Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana,
mpenzi wako akiwa na shida fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na
kama huna mueleze kwamba sina kisha muangalie jinsi gani mnaweza kusaidiana
katika kutatua tatizo linalomkabili.
Itakuwa siyo busara kama utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba ukimweleza mpenzi wako ataona kwamba unamchuna. Wapenzi wanaopendana kwa dhati hawachunani bali wanasaidiana, na hili ni kwa pande zote mbili.
Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na
wakati mwingine unakuta kuchuna kwingine ni kwa mambo ya starehe. Kwa mtu
mwenye mapenzi ya kweli na wewe unadhania atakuchukuliaje? Ni wazi ataona huna
malengo naye bali unataka kumtumia tu. Na akigundua hivyo ni rahisi sana kuamua
kuachana na wewe.
Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya
kutaka kukuomba pesa kila wakati tena katika matumizi mengine ambayo siyo ya
msingi, mbinu zifuatazo ni muhimu kuzifuata:
Kwanza; kama huna pesa wakati mpenzi wako
anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda
ukashindwa kuzitimiza.
Pili; jambo la muhimu ambalo wanaume wengi
wanalisahau ni kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa. Utakuta kila kitu
ananunua yeye, hata nauli ya basi analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake.
Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe
majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna pesa
zinavyokuwa hazitoshi na akaweza kubana matumizi.
Tatu; kuna wanaume wengine tangu wanatongoza
wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa pesa kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza
kumjengea imani mpenzi wako kuwa wewe unazo.
Unachotakiwa mapema ni kudhibiti matumizi
yako hata kama pesa zinakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakushibishi uhitaji,
kadiri unavyotoa ndivyo unavyoongeza mahitaji.
Mwisho naomba niseme kwamba, mapenzi ni
kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku na wewe ukiwa na tatizo
akusaidie.
Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi
hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga mizinga mpenzi wako kila mara kunapunguza
mapenzi hivyo epukana na tabia hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MAMBO MATATU KWA WENYE WAPENZI WACHUNAJI.”
Post a Comment