Monday, November 9, 2015
MKWASA: MPIRA WA SASA HAUNA MWENYEWE
Do you like this story?
Kocha wa Taifa Stars mzawa, Charles Boniface Mkwasa. |
Kocha wa makipa wa Stars, Manyika Peter (kushoto) akiwanoa makipa wake leo jijini Johannesburg. |
Kikosi cha Taifa Stars kikiendeleza tizi, k.utoka kushoto ni kipa Aishi Manula, Nadir Haroub ‘Cannavaro (nahodha), Juma Abdul na Farid Musa. |
Na
Saleh Ally
KIKOSI
cha timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars kimeweka kambi jijini
Johannesburg, Afrika Kusini kujiandaa na mechi dhidi ya Algeria.
Stars
itaivaa Algeria katika mechi ya kuwania kucheza Kombe la Dunia mwaka 2018.
Mechi hiyo itapigwa Novemba 14 jijini Dar es Salaam, kabla ya kurudiana Novemba
17 jijini Algiers.
Katika
kambi ya Stars mjini hapa, karibu kila kitu kimekuwa kikionekana kwenda vizuri
na matumaini ni makubwa kwa Stars itafanya vizuri licha ya ubora wa Algeria.
Bado
inaonekana kuna mgawanyiko kati ya wapenda soka wengi. Wako wanaoamini Algeria
hawawezekani, lakini wako wanaoamini kujituma, kufanya kazi ya ziada,
inawezekana kabisa Stars ikawashangaza wengi.
Championi
Jumatatu, limefanya mahojiano na kocha wa Taifa Stars mzawa, Charles Boniface
Mkwasa kuhusiana na hali ya kambi yake na muendelezo wa mipango.
Kambi
hiyo iliyo katika Hoteli ya Holiday Inn Express iliyo katika ulinzi mkali na
utulivu wa hali ya juu.
Pia
kambi hiyo imeandaliwa mpishi maalum ili kuhakikisha chakula cha wachezaji
kinakuwa salama na wanakula wanachokihitaji.
Championi:
Tuanze moja kwa moja, unaizungumziaje hii kambi ya jijini Johannesburg?
Mkwasa:
Kwa ujumla kambi iko vizuri, iko katika sehemu nzuri na salama. Tunaamini
malengo ambayo tulikuwa tumeweka basi tutayafikia.
Championi:
Mazoezi ambayo umekuwa ukifanya yanaonekana ni makali sana. Unaweza
ukazungumzia kwa maana ya kufafanua, hii maana yake nini?
Mkwasa:
Wachezaji wametokea katika timu tofauti, tumeanza kutafuta ‘fitnesi’ ya
pamoja. Mazoezi ni magumu sana lakini vijana wanaonyesha kujituma na huu ndiyo
wakati mwafaka kufanya hivyo, kadiri siku za mechi zinavyosogea, hauwezi
kufanya hivyo.
Championi:
Lakini wachezaji hao wanatokea katika klabu zao walipokuwa wanacheza ligi. Kuna
haja ya kuwafua kwa nguvu hivyo?
Mkwasa:
Ni kweli wametokea kwenye ligi, lakini tumekuwa tukiwafuatilia kwa karibu
na kuona fitnesi yao inapishana, ndiyo maana tumeamua kutafuta ya pamoja.
Championi:
Algeria ina wachezaji wenye maumbo makubwa, warefu na wanatumia sana mipira ya
juu. Mmejiandaa vipi kupambana na hilo?
Mkwasa:
Mpira kawaida una mipango yake, bahati mbaya wachezaji wetu wengi wana maumbo
madogo. Lakini hauchezwi kwa urefu. Utaona kuna timu zina wachezaji wafupi,
mfano wa Lionel Messi lakini bado wamefanikiwa.
Kumbuka
Hispania, Brazil walikuwa wana wachezaji wengi wafupi na wakabeba Kombe la
Dunia.
Kikubwa
tutajipanga kudhibiti mapema ujio wa mipira ya juu. Vizuri tahadhari kabla ya
hatari.
Championi:
Taifa Stars inaanzia nyumbani, mmejipanga vipi?
Mkwasa:
Hakika mpira wa sasa hauna nyumbani na ugenini. Lakini tumejipanga,
tunajua tunatakiwa kuwa na matokeo mazuri yatakayotulinda mechi ya ugenini.
Championi:
Mechi dhidi ya Nigeria, pia Malawi kikosi chako kilionekana kina makosa ya
umaliziaji. Hili limefanyiwa kazi kweli?
Mkwasa:
Kuna matatizo hauwezi kuyamaliza kwa siku mbili tatu.
Tunaendelea kutengeneza
kila mara tunapokuwa kambini ingawa umakini ungeweza kujengwa zaidi katika
klabu zao kwa kuwa sisi tunakaa na wachezaji kwa muda mfupi sana.
Lakini
hatuchoki, tunalifanyia kazi kila mara (suala la umaliziaji) kuhakikisha mambo
yanakwenda sahihi. Tunaendelea kulikemea, ila halitaisha kwa siku moja tu.
Championi:
Kuna mashabiki hadi sasa wanaamini Tanzania kuifunga Algeria, au kuing’oa ni
ndoto. Hili linakuvunja moyo?
Mkwasa:
Mpira umebadilika sana, haujali nyumbani au ugenini na wala hauendeshwi
tena kwa historia. Tunawaheshimu sana Algeria kutokana na ubora wao. Lakini
tunataka kucheza nao na kushinda.
Championi:
Ndiyo timu bora kabisa kutoka Afrika. Hauoni ni timu hatari kwa kikosi chako?
Mkwasa:
Kweli ni wazuri na bora, tunaheshimu uwezo wao lakini tunachotaka ni kufanya
vema na kushinda na katika mpira kutokana na mabadiliko, inawezekana. Angalia
Iceland imeifunga Uholanzi, kwa sasa mambo hayo ni ya kawaida.
Utaona
mechi na Algeria, wako walioamini tutafungwa tatu au nne. Lakini tukaonekana
ndiyo tulistahili kushinda, lakini hatukuwa makini.
Championi:
Hamkuwa makini, unafikiri mechi ijayo umakini umeongezeka?
Mkwasa:
Kadiri tunavyojifunza, inawezekana kabisa. Wachezaji wasikilize na
kuelewa mafunzo yetu, halafu wayafanyie kazi. Ninaamini itawezekana.
Championi:
Ikitokea umewakosa Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta. Unaamini kikosi
ulichonacho hapa Johannesburg, kinaweza kupambana na Algeria na kushinda?
Mkwasa:
Siwezi kufananisha ujuzi wa kila mmoja binafsi, pia siombi wasiumie. Lakini
katika mpira lolote linawezekana. Tumewachagua vijana tuko nao hapa, ni bora na
wanaweza kucheza ingawa watakosa uzoefu ambao wanao kina Samatta na Ulimwengu
na kweli tunauhitaji sana uzoefu wao. Kwa vijana kupangwa dhidi ya timu kama
Algeria, si kitu kidogo. Wazoefu kama Ngassa na wengine wapo, lakini ninaamini
tutapambana.
Championi:
Mwisho kwa Watanzania wapenda soka, una lolote la kuwaeleza?
Mkwasa:
Sisi tuko hapa tunapambana sana, natamani wangeona kila jambo. Nia yetu ni
kupigania taifa la Watanzania, nao wakiwa ndani. Hivyo siku hiyo waje, vijana
wakiona watu wanawaunga mkono nao wataongeza juhudi zaidi, watajua wana deni.
Nawakumbusha sisi tunafanya kazi kwa niaba yao Watanzania. Waje kwa wingi
tuungane kupambana na Waalgeria ambao watakuwa wakitusubiri kwao kuungana na
mashabiki wao ili watuchanganye.
(PICHA/HABARI
NA SALEH ALLY/ GPL, JOHANNESBURG)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MKWASA: MPIRA WA SASA HAUNA MWENYEWE”
Post a Comment