Friday, December 4, 2015
TAARIFA KWA UMMA TAHADHARI KUHUSU KUINGILIA AU KUFUATILIA MAWASILIANO YA WATU
Do you like this story?
Katika siku za
hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kuwepo kwa Programu (Application) ya simu
ikijulikana kama SOFTBOX TANZANIA iliyosemekana iko kwenye Google PLAYSTORE.
Ilidaiwa kuwa
program (Application) hiyo ya SOFTBOX TANZANIA ilikuwa na uwezo wa kunasa au
kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp
kutoka kwenye simu ya mtu binafsi.
Kwa yeyote
aliyekuwa na nia hiyo ya kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi
pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu mwingine
alihitajika kulipia fedha kiasi cha Tshs 35,000/= kupitia mitandao ya simu ili
kupata namba ya siri kwa ajili ya kuwezesha nia hiyo.
Mamlaka ya
Mawasiliano imefanya uchunguzi kubaini kuwepo kwa programu hiyo na ukweli
kuhusu uwezo wake wa kufanya kilichodaiwa, ikiwa ni pamoja na kuangalia madhara
ya program hiyo na sheria inasema nini kuhusu suala hili.
Baada ya
kufanya uchunguzi wa kina, Mamlaka ya Mawasiliano ilibaini na imejiridhisha
kuwa program (Application) hiyo haina uwezo huo wa kunasa au kuingilia
mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka
kwenye simu ya mtu binafsi kama ilivyodaiwa.
Aidha Mamlaka
imebaini kuwa watengenezaji (Developers) wa programu hiyo walikuwa na nia ya
kutapeli na kujipatia fedha hiyo kiasi cha Tshs 35,000/= kwa njia ya
udanganyifu wakitumia kivutio cha kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu,
ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu za watu
binafsi.
Programu
(Application) nyingine ya aina hiyo iliibuka tena ikiitwa SIMNET Tanzania ikiwa
na maelezo kama ya awali.
Wakati Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania pamoja na Jeshi la Polisi wakiendelea na uchunguzi
zaidi, tunapenda kuuarifu umma wa Watanzania kuepuka kufanya mambo yafuatayo:
1.
Kuvutiwa na matendo yaliyo kinyume
na sheria na maadili ya matumizi mazuri ya mawasiliano kama hili la kunasa au
kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp
kutoka kwenye simu ya mtu binafsi.
2.
Kitendo hiki ni
kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 6 na 10 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao
ya Mwaka 2015 na kifungu cha 123 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na
Posta (EPOCA) ya Mwaka 2010.
Sheria katika
vifungu hivyo inakataza mtu yeyote kuingilia mawasiliano ya mtu mwingine.
Adhabu kali ya makosa haya ni faini isiyopungua shilingi milioni tano au
kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
3.
Mamlaka inawatahadharisha watumiaji
wa huduma za mawasiliano kutokuwa wepesi na kudanganyika kufanya malipo yoyote
kwa njia ya mitandao kwa huduma wasiyokuwa na uhakika nayo au bila kujiridhisha
na uwepo wa huduma hiyo.
4.
Ni vizuri kutoa
taarifa kwa mtoa huduma wako au kuwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano kupitia
barua pepe malalamiko@tcra.go.tz au kupiga simu namba 0784558270/1.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania
04/12/2015.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ TAARIFA KWA UMMA TAHADHARI KUHUSU KUINGILIA AU KUFUATILIA MAWASILIANO YA WATU”
Post a Comment