Thursday, March 17, 2016
MKUU WA SHULE ASIMAMISHWA KAZI KWA TUHUMA ZA NGONO.
Do you like this story?
Mkuu wa wilaya ya
Mkalama, Christopher Ngubiagai ameagiza mkuu wa Shule ya Sekondari Chemchem,
Tarafa ya Kirumi, Juma Makoro, asimamishwe kazi mara moja, ili kupisha
uchunguzi dhidi ya tuhuma inayomkabili ya kufanya vitendo vya ngono na
wanafunzi wake wa kike.
Mkuu huyo wa wilaya,
ametoa agizo hilo juzi wakati akizungumza kwenye kikao cha utendaji
kilichohudhuriwa na watendaji wa vijiji, kata, tarafa na waratibu elimu kata
kilichofanyika kwenye ghala la kijiji cha Nduguti.
Ngubiagai amemwagiza
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkalama Machi 17 mwaka huu
amwandikie barua ya kumsimamisha kazi mkuu huyo wa shule ili apishe uchunguzi
wa tuhuma dhidi yake.
“OCD, (huku akiwa
amemwangalia) hakikisha kuanzia sasa mwalimu Makoro anakamatwa na kufanyiwa
uchunguzi wa kina juu ya tuhuma ya vitendo vyake ambavyo ni kinyume na maadili
ya kazi yake,” alisema Mkuu huyo wa wilaya na kuongeza;
“Mkuu wa TAKUKURU na
wewe kwa nafasi yako, hakikisha unachunguza tuhuma ya mkuu huyo wa Shule ya
Sekondari Chemchem. Serikali ya awamu ya tano haina kabisa nafasi na watumishi
wa umma wenye tabia mbaya ikiwemo ya kuwaharibia maisha wanafunzi wa kike”
Akifafanua alisema
kwa muda mrefu mwalimu Makoro amekuwa akituhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi
wa kike ambao ni sawa na watoto wake wa kuzaa.
“Inadaiwa mwalimu
Makoro amekuwa akiagiza mwanafunzi wa kike ampelekee madaftari ofisini kwake na
mwanafunzi akikabidhi madaftari hayo anamlazimisha ampige busu hii ni
aibu kubwa sana,” alisema kwa masikitiko makubwa.
Katika hatua
nyingine, Ngubiagai ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba, alisema
kwamba amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Iramba, kutoa maelezo
ya kueleweka ni kwanini ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike Shule ya Sekondari
Kinyangiri haujakamilika toka ujenzi wake uanze Septemba, 2011.
“Mkuu wa Shule ya
Sekondari Kinyangiri kwa ubunifu wake, aliandika andiko la kuomba ufadhili kwa
kutoka ubalozi wa Japan kujengewa bweni la wanafunzi wa kike, andiko hilo
lilizaa matunda Septemba 6, 2011 kwa ubalozi huo kutoa hundi ya shilingi
118,686,817,” alisema.
Alisema kwa sababu
zisizojulikana hundi hiyo iliyopokelewa na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji kwa
wakati huo na kukaa nayo miezi minne bila kuipeleka benki.
“Baada ya miezi hiyo
minne ya kukaa na hundi hiyo kwenye droo ya meza ya ofisi ya mkurugenzi
mtendaji, aliipeleka benki na baada ya kuingiza kwenye akaunti, pia akakaa nayo
kimya kwa zaidi ya miezi minne mingine, ndipo akampa mkandarasi kazi imechukua
zaidi ya miaka minne hadi sasa na haijakamilika,” alisema Ngubiagai.
Alisema ubalozi wa
Japan ulitoa masharti kwamba wenyewe utajenga bweni, halmashauri inunue vitanda
80 na mashuka 80 na wananchi wachangie kuleta maji, kokoto na mchanga na
halmashauri hadi sasa haijatimiza wajibu wake.
Wakati huo huo,
alisema kuwa kwenye fedha za ufadhili kutoka Japan kuna dalili kubwa ya
ubadhirifu ambao kwa sasa anaufanyia kazi.
Kwa mujibu wa DC
Ngubiagai, Mkuu huyo wa Shule ya Sekondari ya Kinyangiri, alifikia uamuzi wa
kuandika andiko la kuomba ufadhili wa kujengewa bweni hilo baada ya wanafunzi
wa kike waliokuwa wamepanga kwenye nyumba za watu binafsi, wengi kujazwa mimba
na kupelekea kuacha Shule.
Na Nathaniel Limu,
Mkalama
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MKUU WA SHULE ASIMAMISHWA KAZI KWA TUHUMA ZA NGONO.”
Post a Comment