Tuesday, March 15, 2016
WAZIRI MKUU AMPA KATIBU TAWALA WA KAGERA SIKU TANO 5 TU.
Do you like this story?
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua hospitali ya rufaa ya
mkoa wa Kagera na kumpa siku tano Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Adam
Swai amletee taarifa juu matumizi ya sh. Milioni 80 ambazo ni fedha za UKIMWI.
Pia amemtaka ifikapo Machi 20, nwaka huu awasilishe taarifa
nyingine ya matumizi ya sh. Milioni 40 za ukarabati wa jengo la wagonjwa maalum
(Grade A)
Ametoa agizo hilo leo asubuhi (Jumanne, Machi 15,
2016) wakati akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo baada ya kutembelea
maeneo kadhaa yakiwemo wodi ya watoto, wodi ya wazazi, chumba cha wagonjwa
mahututi (ICU ) na chumba cha kuhifadhia maiti.
"Kulikuwa na frsha za ukimwi sh. Milioni 80 ambapo kila
mtumishi alipaswa kupata sh. 200,000/- lakini ninyi mmewapa sh. 80,000 /-. RAS
fedha hizi zimeenda wapi? Nataka uniletee taarifa ofisini kwangu Dar es
Salaam ifikapo tarehe 20 mwezi huu," alisema huku akishangiliwa.
"Kwa mujibu wa taarifa ya CAG pale grade A kuna mgogoro
wa sh. milioni 40. Wewe taarifa unayo lakini hujaifanyia kazi yoyote.
Nataka tarehe 20 nayo hii pia niipate na nione umetoa mapendekezo gani."
Kuhusu tatizo la madaktari katika hospitali hiyo, Waziri
Mkuu alisema atawasiliana na Waziri wa Afya ili madaktari watano ambao
wanasubiri ajira rasmi lakini wameanza kazi kwa mkataba hospitali hapo wapewe
ajira rasmi. Pia alisema amebaini upungufu wa madaktari bingwa uliopo katika
hospitali hiyo.
Pia aliahidi kufuatilia maombi yao ya gari la wagonjwa hasa
ikizingatiwa kuwa anayo maombi kama hayo kutoka hospitali za Mawenzi
(Kilimanjaro), na Ligula (Mtwara).
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwapongeza
watumishi wa hospitali hiyo kwa huduma zao nzuri wanazotoa kwa wagonjwa.
"Nineridhishwa na kauli walizotoa wagonjwa juu yenu. Tofauti na hospitali
nyingine nilizopita, wao wamesema hawajatozwa fedha ili wapatiwe dawa.
Nimefarijika sana."
"Endeleeni kuwa na huruma kwa wagonjwa. Endeleeni kuwa
na lugha nzuri kwa wagonjwa. Hawa wagonjwa hawakuogopa kuelezea hisia zao.
Wamesema kwa uwazi kabisa kwamba mnawajali," alisema.
Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu,
Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Thomas Rutachunzibwa alisema hospitali hiyo
inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa pamoja na madaktari wa
kawaida.
"Tunao madaktari 10 lakini wanaohitajika ni 30. Tunao
madaktari wasaidizi wanane lakini wanaohitajika ni 23 na madaktari bingwa
waliopo ni watatu tu lakini wanaohitajika ni 24. Tunaomba tupatiwe watumishi
hawa ili tuweze kutoa huduma kulingana na matarajio ya wananchi wetu," alisema.
Akifafanua kuhusu mahitaji ya hospitali hiyo, Dk.
Rutachunzibwa alisema wanahitaji sh. bilioni 1.8 kwa mwaka bila ya kuweka
mishahara ili waweze kufanya kazi yao kwa umakini.
"Tunahitaji sh. milioni 802 kwa ajili ya matumizi ya
kawaida lakini tunachopokea hivi sasa ni sh. milioni 299 ambayo ni sawa na
asilimia 30 ya mahitaji yetu."
"Bajeti ya dawa tuliyotenga ni sh. milioni 960 lakini
tunapokea sh. milioni 143 ambazo kiuhalisia zinatosha kwa matumizi ya miezi
miwili tu. Tumelazimika kufanya marekebisho ya bei za dawa kwa ridhaa ya Bodi
ya hospitali ili tuweze kumudu kutoa huduma kwa wananchi,"alisema.
Alisema ili kubana mianya ya upotevu wa mapato, wanahitaji
kuwa na kompyuta 15 lakini hadi sasa wamefanikiwa kununua kompyuta mbili tu
ambazo ziko Grade A na idara ya wagonjwa wa nje (OPD) ili kuimarisha utaratibu
wa ukusanyaji mapato.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, MACHI 15, 2016.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MKUU AMPA KATIBU TAWALA WA KAGERA SIKU TANO 5 TU.”
Post a Comment