Tuesday, March 15, 2016
WAZIRI MKUU AMWAGIZA CAG AENDE BUKOBA HARAKA KUMALIZA MGOGORO WA VIWANJA.
Do you like this story?
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
aende Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kufanya upya tathmini na kukagua ugawaji
wa viwanja 843 kwenye manispaa hiyo.
Waziri Mkuu
Majaliwa alitoa agizo hilo jana (Jumatatu, Machi 14, 2016) wakati akihutubia
maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa
Mashujaa wa Mayunga mjini Bukoba.
Alifikia hatua
hiyo baada ya wananchi kubeba bango lenye ujumbe kuelezea kutopewa viwanja
hivyo vilivyopimwa na Manispaa ya Bukoba.
Viwanja hivyo
vilipimwa na kugawiwa kwa wananchi ambao baadhi yao baada ya kulipa fedha,
hawajapewa viwanja hivyo ikiwa ni takriban miaka zaidi ya 10.
Akiwa katika
siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kagera, Waziri Mkuu alilazimika kumpandisha
jukwaani Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Bw. Wallace Karia ili atoe
maelezo ya nini kimekwamisha wananchi kupewa viwanja hivyo.
Katika maelezo
yake, Bw. Karia alisema mwaka 2003, vilitengwa viwanja 843, kati ya hivyo 352
vilikuwa eneo la Kyabitembe, 137 Ihungo na Rwome na vingine 132.
Bw. Karia
ambaye hana muda mrefu tangu ahamishiwe katika manispaa hiyo, alisema
kumbukumbu za ofisi zinaonesha kuwa viwanja 182 ndio wahusika hawajapewa, na
viwanja vingine 85 vilikuwa havijapimwa eneo la Kilimahewa na Kashai, huku
kukiwa na vingine 5,000 vya mradi.
Aliongeza kuwa
walitarajiwa kuwalipa wananchi hao katika mwaka wa fedha 2016/17; kauli ambayo
ilisababisha kelele kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa Waziri
Mkuu.
Kutokana na
hilo, Waziri Mkuu aliingilia kati na kumueleza Mkurugenzi huyo kuwa kelele hizo
zinaashiria kuwa watu hao hawajaridhishwa na majibu yake.
Alisema
anafahamu kuwa mkurugenzi huyo na meya ni wapya, lakini akawaagiza ndani ya mwezi
mmoja, kufanya mapitio ya viwanja hivyo 843, na hasa watu 182 ambao
hawajapatiwa viwanja wahakikishe wanawapatia kwa sababu viwanja vipo.
“Rais
mstaafu alikuja hapa na kupewa kilio cha kupunjwa fedha. Najua wakati huo
mtasema ninyi hamkuwepo. Wewe (MD) na Meya wako mkae na kupitia mikataba na
mafaili.
Nyie na mkoa mkae pamoja na kujua vile viwanja vilivyochukuliwa na
JWTZ. Nitamleta CAG hapa, ndani ya mwezi mmoja afanye mapitio ya viwanja tu,” alieleza Waziri Mkuu na kushangiliwa na maelfu ya wananchi.
Katika mkutano
huo, Waziri Mkuu pia aliwahakikishia wakazi wa Manispaa ya Bukoba kuwa
watalipwa fidia zao baada ya kukubali kupisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji
wenye thamani ya sh. bilioni 31.
Waziri Mkuu
aliendelea na ziara yake ya siku tatu mkoani Kagera kwa kutembelea wilaya za
Misenyi na Karagwe na leo atakuwa wilayani Ngara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MKUU AMWAGIZA CAG AENDE BUKOBA HARAKA KUMALIZA MGOGORO WA VIWANJA.”
Post a Comment