Wednesday, May 25, 2016
MOURINHO NI MTU SAHIHI WA KUIRUDISHA MANCHESTER UNITED KWENYE UBORA WAKE?
Do you like this story?
Na
Mahmoud Rajab
Muda
na wakati wowote kutoka sasa Manchester United watamtangaza Jose Mourinho kama
kocha mpya wa timu hiyo.
Watu wengi
wanaamini ujio wa Mourinho kwenye klabu ya Manchester United si sahihi kutokana
na pande zote kuwa na falsafa zinazotofautiana.
Lakini
kikubwa kinachomleta Mourinho United si kingine bali na makombe tu. Hilo ndilo
suala ambalo limekuwa likiwatesa United kwa kipindi kirefu tangu kuondoka kwa
Sir Alex Ferguson. Ikumbukukwe kuwa United wamekuwa wakisuasua kiasi cha kukosa
matokeo hata kwa timu dhaifu, kitu ambacho huko nyuma hakikuwa kikitokea mara
kwa mara.
United
wameshinda kombe la FA, hilo ni jambo jema lakini si kwa kiwango cha
kuwasahaulisha mashabiki na machungu wanayopitia kwa sasa. Wamekuwa ni wa
kiwango cha kawaida sana kwa miaka takribani miwili iliyopita. Si rahisi hata
kidogo kwao kunyanyua mdomo na kupinga ujio wa Jose Mourinho klabuni hapo.
Ni
ukweli usiopingika kuwa Mourinho ana mapungufu yake ikiwemo kuingia katika
rapsha za hapa na pale na waandishi, makocha wenzake, marefa pamoja na maafisa
wa FA. Lakini mbali ya yote hayo yeye ni mtu sahihi wa kuifanya United kurudi
katika ubora wao. Huyu ni kocha mwenye njaa ya ushindi wakati wote.
Ana
rekodi ya kushinda mataji katika nchi zote nne alizowahi kupita kufundisha
soka. Ameshinda ligi ya mabingwa mara mbili-amefanya hivyo akiwa na FC Porto ya
Ureno pamoja na Inter Milan tena katika sehemu zote hizo akishinda makombe
matatu kwa mpigo (treble).
Achana
na uwezo wake wa kuvikusanya vikombe vya ndani kama FA, Capital One na
kadhalika, huyu ni mtu mwenye asili ya upambanaji na asiyetaka masihara kwenye
kazi kitu ambacho United ndicho wanakitaka haswa.
United
wanamhitaji kwa sababu ya kuwapa mashabiki, washika dau na hata wachezaji imani
na kuweza kutemebea vifua mbele ya wapinzani wao kama vile mahasimu wao wakubwa
wa jiji la Manchester, Manchester City ambao msimu ujao watakuwa chini ya Pep
Guardiola.
Wanamhitaji
Mourinho kuhakikisha kuwa hayatokei kama ya Liverpool kwamba kucheza UEFA kwao
imekuwa ni kama bahati.
Ujio
wa Mourinho United ni pigo kubwa kwa mashabiki wa vilabu vingine. Kamwe
wasingependa kumwona akirejea na kutua United kwa sababu wanajua fika United
iliyo chini ya Van Gaal ingeendelea kuwa ya kawaida na isiyoleta hofu yoyoye
kwa timu pinzani, lakini Mreno huyo ataifanya United iwe ni timu yenye
kupigania ubingwa kwenye kila michuano inayoshiriki kama ilivyokuwa katika
nyakati za Sir Alex Ferguson.
Ni
ukweli usiopingika kwamba staili ya mpira wa Mourinho si ya kuvutia wala
kusisimua.
Lakini
anajua vizuri namna gani ya kuirudisha timu kwenye mstari pale inapopotea. Kitu
kizuri kwake ni kwamba si mtu mwenye kutaka sifa ya kucheza mpira wa kuvutia
pale anapoona mpinzani wake amemzidi mbinu bali hutumia mbinu mbadala ili
kumdhibiti mpinzani wake.
Akiwa
na klabu ya Real Madrid miaka takriban sita iliyopita, mchezo wake wa kwanza
dhidi ya Barcelona, alifungwa mabao 5-0. Mwaka mmoja baadaye akawafunga bao 1-0
na kunyanyua ndoo ya Copa Del Rey ambayo ndio ilikuwa ya kwanza akiwa nchini
humo (ya kwanza kwa Madridi tangu msimu wa 2007-8).
Ukweli
ni kwamba hata mashabiki wa timu kama ya Arsenal wangependa kuwa na kocha wa
aina yake hasa baada ya kupita miaka mingi bila timu yao kunusa mafanikio.
Mwaka
mmoja baadaye akiwa hapo hapo Madrid aliifunga Barca ya Pep akielekea kubeba
ndoo ya La Liga. Huo ulikuwa ni ushindi wao wa kwanza kwa mahasimu wao hao
wakubwa katika soka la Hispania kwa takriban miaka minne na ushindi wa kwanza
katika dimba la Nou Camp kwa miaka mitano.
Alivunja
rekodi ya ufungaji kwa klabu kwenye ligi baada ya kuiongoza kufunga magoli 109.
Mourinho
ndiye aliyeipa ubingwa wa kwanza Chelsea baada ya miaka 50 wakipata pointi
ambazo hawakuwahi kupata tangu kuanzishwa kwa timu hiyo.
Vivyo
hivyo kwa upande wa Inter Milan, walikuwa wakipata mfululizo wa matokeo ya
kawaida chini ya kocha Roberto Mancini. Mourinho alipochukua timu tu aliipa
ubingwa wa UEFA, Serie A na kombe la ligi. Kwa maana nyingine alichukua makombe
matatu kwa mpigo (treble)
Tangu
alipoondoka Chelsea, timu hiyo ilitwaa ubingwa wa EPL mara moja ikiwa chini ya
Carlo Ancelotti mpaka alivyorudi msimu wa 2013/14 na kuchukua ndoo ya EPL msimu
wa 2014/15 na kombe la Capital One.
Hii yote
inadhihirisha kwamba Mourinho ni mtu sahihi wa kuirudisha United katika ubora
wake.
Na
ndiyo maana licha kupata matokeo mabovu msimu huu ulioisha lakini mashabiki wa
Chelsea bado walikuwa na imani naye kutokana na kuamini kwamba alikuwa ni mtu
sahihi wa kuipeleka mbeke klabu yao
Ni
figisu tu za wachezaji ndizo zilizomng’oa Mourinho Chelsea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MOURINHO NI MTU SAHIHI WA KUIRUDISHA MANCHESTER UNITED KWENYE UBORA WAKE?”
Post a Comment