Sunday, May 29, 2016
MUHONGO AITUMBUA KAMPUNI ILIYOINGIZA MAFUTA FEKI NCHINI.
Do you like this story?
SERIKALI
imemsimamisha msambazaji wa mafuta Kampuni ya Sahara Energy Resourses
Limited ya Nigeria aliyeingiza mafuta ya ndege (JET A1) yaliyochafuka na
kumtaka kusafisha matangi pamoja na mabomba ya mafuta ya kampuni
zilizopokea mafuta hayo.
Aidha,
imeelezwa pamoja na kutokea kwa tatizo hilo la kuchafuka kwa mafuta
hayo nchi haitaingia katika ukosefu wa nishati hiyo muhimu kwa kuwa kuna
akiba ya kutosha kwa siku 14 na tayari kampuni ya Puma imeagiza mafuta
ambayo yataingia nchini Juni 7, mwaka huu.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa kauli hiyo jana
wakati alipotembea kampuni za mafuta zilizopokea mafuta yaliyochafuka
kwa kuchanganyika na petroli jijini Dar es Salaam ili kubaini ukweli wa
uhaba wa mafuta ya ndege.
Profesa
Muhongo aliiagiza kampuni hiyo ya Sahara Energy Resources Limited ya
Nigeria kuhakikisha inasafisha matangi pamoja na mabomba ya mafuta
kuanzia leo na kama haitatekeleza hilo itakuwa ni mwisho kufanya kazi
nchini.
“Msafishe
haya matenki pamoja na mabomba yote kwa gharama zenu. Haya ni maagizo
sisi hatuwezi kuendelea kusubiri, hamuwezi mkasababisha nchi ikawa na
uhaba wa mafuta kwa majadiliano yenu ambayo hayana mwisho.
“Usafishaji
unatakiwa kuanza kesho, kama hautafanyika kuanzia hiyo kesho, basi
Sahara isahau kufanya biashara katika nchi hii. Na sio hilo tu hata
tenda (zabuni) alizokuwa amepata nazo tutazifuta,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema
kuwa kampuni hiyo haitakiwi kupewa zabuni nyingine hadi hapo uchunguzi
utakapokamilika wa kubaini ukweli wa mafuta hayo kuchafuka kwa
kuchanganyika na petroli.
Profesa
Muhongo alisema hatua walizochukua ya kwanza ni kumsimamisha
kujihusisha na zabuni yoyote itakayotangazwa kuanzia sasa lakini pia
kutakiwa kusafisha matangi na mabomba hayo.
Aliongeza
kuwa hii ni mara ya pili kwa kampuni hiyo mafuta yake kuwa na tatizo
kwani mara ya kwanza mafuta yake yalibainika kuwa machafu akarudishwa
nayo.
Awali
mwakilishi wa kampuni hiyo ambaye yuko hapa nchini alisema, hawana
sehemu ya kuhifadhi mafuta hayo ambayo yamechafuka hivyo wanasubiri meli
yao irudi ili waweze kuyaondoa mafuta.
Hata
hivyo, kampuni ya kuhifadhi mafuta nchini ya Tanzania International
Petroleum Reserves Limited (TIPER) ilimhakikishia Profesa Muhongo kuwa
wana nafasi ya kuhifadhi mafuta yote yaliyochafuka, hatua ambayo waziri
huyo aliiagiza kampuni hiyo kuhifadhi mafuta hayo katika matangi ya
TIPER badala ya kusubiri meli.
“Hilo
linatuchelewesha TIPER wameshakubali wana nafasi ya kuhifadhi hayo
mafuta, kwa hiyo yahifadhi hapa ili msafishe hayo matenki, ili mafuta
yatakayokuja yakute matenki ni masafi,” alisema.
Aidha,
alisisitiza kuwa taifa haliwezi kuingia kwenye uhaba wa mafuta ya ndege
na yapo ya kutosha siku 14 kwani kampuni ya Puma tayari imeshaomba
mafuta kutoka katika kampuni za Total na SP ya Rwanda.
Pia meli ya Puma itaingia nchini Juni 7 na meli nyingine itaingia Juni 13.
Awali
akizungumzia hali hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uagizaji
Mafuta kwa Pamoja, Michael Mjinja alisema, meli hiyo iliingia nchini
Mei 5, mwaka huu na mafuta hayo yalithibitishwa kuwa na ubora na Shirika
la Viwango nchini (TBS).
Alisema
baada ya mafuta hayo kushushwa ilibainika kuwa yamechafuliwa hatua
iliyowafanya kumuagiza aliyeleta mafuta hayo kuyaondoa.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji
(EWURA) Felix Ngamlagosi alisema, kwa sasa kuna mafuta ya kutosha kwa
siku 14 lakini kuna hatua nyingine zinazochukuliwa ili kuhakikisha
hakuna uhaba wa mafuta utakaotokea.
“Hayo
yaliyochanganyika kuna hatua zinazochukuliwa ikiwa ni pamoja na
kuchukua sampuli za pamoja na sisi ni wasimamizi ili kuhakikisha
zinapelekwa maabara na kujua kitu gani kilitokea,” alisema.
Profesa
Muhongo alizitembelea kampuni hizo ambazo ni Puma Energy, Gapco
Tanzania Ltd, Oilcom, ORXY Energies na TIPER. Meneja wa Huduma za
Usafiri wa Anga wa Oilcom, Haruna Magota alimwambia Waziri Muhongo kuwa,
mafuta waliyopokea yalikuwa ni lita milioni 8.8 na wao walikuwa na lita
milioni 2.6, ambapo mafuta hayo yote yameharibika.
Alisema
ukosefu wa mafuta hayo umekuwa ni tatizo kwa wateja wao ambao ni
mashirika ya ndege kwani jumla ya lita milioni 10.8 yote yamechafuka.
Aidha
aliongeza kuwa wakaguzi wa meli walishawahi kutoa onyo kwa kampuni hiyo
kuwa meli zake hazina viwango vinavyotakiwa vya kubeba nishati hiyo.
Aidha
kampuni za kuagiza mafuta nchini zilitaka kampuni ya Sahara Energy
Resources Ltd ya nchini Nigeria kuweka hadharani uthibitisho wa
kuhujumiwa kuhusiana na kashfa ya uingizaji mafuta ya ndege machafu hapa
nchini inayolikabili shirika hilo.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Chama cha Waagizaji Wakubwa wa Mafuta ya Petroli
nchini (TAOMAC) iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari jijini Dar es
Salaam juzi, waagizaji hao waliitaka kampuni hiyo kutaja jina la kampuni
au mhusika yeyote anayeaminika kuihujumu kampuni hiyo kama ambavyo
imenukuliwa na vyombo vya habari nchini ikijitetea kupinga kashfa hiyo.
“Tunawaomba
wenzetu hawa wahakikishe wanakabidhi jina la kampuni au mtu yeyote
wanayemshuku kuwa anahusika na kashfa inayowakabili kwa Jeshi la Polisi
au chombo chochote cha usalama nchini vinginevyo sisi tutaamini kuwa
utetezi wao ni uwongo na unalenga kutafuta njia ya kutokea,’’ alisema Mkurugenzi Mtendaji wa TAOMAC, Salum Bisarara kupitia taarifa hiyo.
Sakata
la kuingizwa kwa mafuta machafu ya ndege aina ya Jet A1 na hofu ya
kukosekana kwa mafuta hayo nchini liliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini
(ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe wakati akichangia hotuba ya bajeti ya
Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017, alisema mafuta
hayo yatakosekana kutokana na kampuni moja ya kigeni iliyopewa zabuni
kuagiza mafuta hayo, kuingiza mafuta ambayo hayawezi kutumiwa na ndege.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MUHONGO AITUMBUA KAMPUNI ILIYOINGIZA MAFUTA FEKI NCHINI.”
Post a Comment