Thursday, May 26, 2016
WANAFUNZI 489 WABAINIKA KUJIUNGA NA CHUO KIKUU BILA KUWA NA SIFA, YADAIWA WALIPATA DARAJA 4.32 KIDATO CHA NNE
Do you like this story?
Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amevunja Kamisheni ya
Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kuwasimamisha kazi mara moja viongozi wake wanne
waandamizi kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasiokuwa na sifa.
Mbali
ya viongozi hao, Mwenyekiti wa TCU, Awadhi Mawenya naye amesimamishwa kwa kosa
la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliobainika kuwadahili wanafunzi
hao.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini hapa, Profesa Ndalichako alitaja tuhuma
zinazowakabili viongozi hao huku akiteua watu wawili kusimamia shughuli za tume
hiyo kwa muda.
Profesa
Ndalichako ambaye Februari mwaka huu alisitisha mkataba wa Mkurugenzi Mkuu wa
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), George Nyategi na kuwasimamisha kazi
wakurugenzi wengine watatu kwa madai ya ukiukwaji wa utoaji wa mikopo pamoja na
ucheleweshaji usio na sababu za msingi, alisema Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa
Yunus Mgaya amesimamishwa kwa kushindwa kusimamia kazi za Tume hiyo ikiwa na maana
kwamba ameshindwa kutekeleza wajibu wake kama mtendaji mkuu wa taasisi.
Mwingine
aliyesimamishwa ni Mkurugenzi wa Ithibati na Uhakiki Ubora, Dk Savinus Maronga
kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya vyuo
vikuu.
Mkurugenzi
wa Udahili na Nyaraka, Rose Kishweko naye amekumbwa katika kadhia hiyo akidaiwa
kudahili wanafunzi wasio na sifa. Pia aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, Kimboka
Istambuli naye amesimamishwa.
Walioteuliwa
na Profesa Ndalichako kusimamia Tume hiyo kwa muda ni Naibu Makamu Mkuu Chuo
Kikuu Ardhi (Utawala na Fedha), Profesa Eleuther ambaye atakuwa Kaimu Katibu
Mtendaji na Dk Kokubelwa Moleli ambaye atakuwa Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na
Nyaraka. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mratibu wa Idara ya Elimu ya Juu Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa
Ndalichako alisema wanafunzi waliodahiliwa walipata daraja (division) 4.32
lakini wakajiunga na chuo kikuu na kupewa mikopo. Wanafunzi hao wametakiwa
kurudisha jumla ya Sh784 milioni huku wakikosa sifa za kusoma ualimu hata wa
ngazi ya cheti.
Alisema
Chuo Kikuu cha St Joseph kilikuwa kimedahili wanafunzi 424 wasiokuwa na sifa za
kujiunga na elimu hiyo lakini pamoja na Serikali kuagiza TCU kuwachukulia hatua
waliohusika, hakuna kilichofanyika.
“Serikali
iliamua kusitisha masomo ya wanafunzi hao lakini hata hivyo, wizara iliendelea
na ukaguzi na mpaka sasa wanafunzi 489 wamebainika kusoma katika chuo hicho
bila ya kuwa na sifa za kujiunga na chuo kikuu,” alisema.
Source:Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WANAFUNZI 489 WABAINIKA KUJIUNGA NA CHUO KIKUU BILA KUWA NA SIFA, YADAIWA WALIPATA DARAJA 4.32 KIDATO CHA NNE”
Post a Comment