Sunday, July 10, 2016
INDIA NA TANZANIA ZASAINI MKATABA WA DOLA MILLIONI 92, MIJI 17 KUPATA MAJI SAFI
Do you like this story?
Serikali ya India na
Tanzania zimesaini mikataba ya miradi ya maendeleo katika sekta za maji,
kilimo, viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano na afya katika kuimarisha
mahusiano ya nchi hizo mbili ili kusaidia wananchi wake.
Mikataba hiyo
imesainiwa leo, wakati Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi alipokua
akifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mikataba wa kwanza
uliosainiwa inahusisha mradi wa kusambaza maji katika mikoa ya Pwani na Dar es
Salaam.
Aidha, mkataba wa
pili unahusisha mradi wa kusambaza maji Zanzibar ambao unatarajiwa kugharimu
dola za kimarekani milioni 92 ambapo mradi huo unatarajiwa kufikia miji 17
nchini na mkataba mwingine utahusisha mafunzo ya ufundi yatakayosaidia
kuzalisha wataalamu mbalimbali.
“Lengo letu ni
kusaidiana na kuimarisha mahusianao yetu katika kukuza uchumi na kutengeneza
fursa mpya za ajira kwa wananchi wetu,” alisema Waziri Modi.
Waziri Modi aliongeza
kuwa Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika
masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa biashara na
hatimaye kukuza uchumi wa nchi hizo.
Kwa upande wake, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alisema Serikali India
imekua na ushirikiano mzuri na Tanzania hasa katika masuala ya maendeleo ambapo
imeweza kuwekeza nchini kiasi shilingi za Kimarekani dola bilioni 2.4 na
kuzalisha ajira 54,176.
Baadhi ya misaada
iliyotolewa na Serikali ya India ni pamoja na mashine ya vipimo vya ugonjwa wa
kansa katika hospitali ya Bugando, itakayosaidia wakazi wa kanda ya ziwa na
nchi nzima kwa ujumla pamoja na kuongeza na kuimarisha ushirikiano kati ya
Shirika la viwanda vidogo vigodo la India kushirikiana na Tanzania katika
kukuza viwanda vidogo na vya kati nchini.
Katika masuala ya
teknolojia ya habari na mawasiliano, Serikali hiyo imeahidi kuleta wataalamu
wao nchini Tanzania kwa lengo la kutengeneza program mbalimbali ili kuisaidia
Tanzania katika masuala ya ulinzi wa mitandao pamoja na kutengeneza namna bora
za ukusanyaji wa mapato ya nchi.
Katika masuala ya
viwanda, Serikali ya India imeahidi kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa za
binadamu zitakazotibu magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria, figo na kisukari,
ikiwa ni pamoja na kutengeneza vifaa tiba vitakavyotumika katika hospitali
mbalimbali nchini kwa lengo la kupunguza gharama ya kununua vifaa hivyo nje ya
nchi.
Aidha, Rais Magufuli
alisema kuwa nchi ya India ina uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo hasa jamii ya
kunde hivyo akawataka wakulima kutumia fursa hiyo kuzalisha mazao hayo kwa
wingi.
“India inauhitaji wa
tani 200 za mazao jamii ya kunde, wakulima mnatakiwa kuzalisha mazao hayo kwa
wingi kwa vile tayari kuna soko la uhakika, na tutahakikisha madalali hawatakuwepo
ili mkulima asikandamizwe” alisema Rais Magufuli.
Katika sekta ya
uwekezaji nchini, India ni nchi ya tatu kwa uwekezaji Tanzania ikifuatiwa na
Uingereza pamoja na China.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ INDIA NA TANZANIA ZASAINI MKATABA WA DOLA MILLIONI 92, MIJI 17 KUPATA MAJI SAFI”
Post a Comment