Monday, July 25, 2016
RAIS MAGUFULI AWASIHI WATANZANIA KUDUMISHA AMANI, UMOJA NA UTULIVU, ASISITIZA SERIKALI KUAMIA DODOMA
Do you like this story?
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewasihi watanzania
kuwaenzi Mashujaa kwa kudumisha Amani, Umoja na Utulivu uliojengwa na mashujaa
hao.Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa
maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa, yaliyofanyika katika uwanja wa
Mashujaa Mjini Dodoma.
Pamoja na
kutoa rai hiyo Rais Magufuli ameahidi kuwa atahakikisha azma ya Serikali
kuhamia Dodoma inatekelezwa kabla ya kuisha kwa kipindi chake cha uongozi wa
miaka mitano.
"Tunapoadhimisha
siku ya Mashujaa hatuwezi kumsahau Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa alisema makao makuu yawe Dodoma, haiwezekani
sisi watoto wake, sisi wajukuu wake tupinge kauli ya Mzee huyu.
"Kwa
hiyo nilikwishazungumza na leo narudia hili katika siku ya Mashujaa,
mlinichagua ndugu zangu wa Dodoma kwa kipindi cha miaka mitano, hadi sasa miezi
minane imepita, nimebakiza miaka minne na miezi minne, nataka kuwathibitishia
kuwa katika kipindi cha miaka minne na miezi minne iliyobaki nitahakikisha
serikali yangu pamoja na mimi tunahamia Dodoma bila kukosa" Amesema Rais
Magufuli.
Kufuatia
maelekezo hayo ya Mhe. Rais, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Kassim Majaliwa ameagiza Mawaziri wote waanze mara moja kuhamia Dodoma na
kwamba yeye mwenyewe atakuwa amehamia Dodoma ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Viongozi
wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed
Shein, Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Mke wa Rais Mama
Janeth Magufuli, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Tulia Ackson, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Mawaziri
Wakuu wastaafu Mhe. John Samwel Malecela na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda,
Mabalozi na wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali, Viongozi wa vyombo vya
ulinzi na usalama, Viongozi wa vyama vya siasa na dini, maafisa na askari
waliopigana vita mbalimbali.
Gerson Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
25 Julai,
2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ RAIS MAGUFULI AWASIHI WATANZANIA KUDUMISHA AMANI, UMOJA NA UTULIVU, ASISITIZA SERIKALI KUAMIA DODOMA”
Post a Comment