Monday, July 18, 2016

VIONGOZI WA DINI WAKWEPA KODI WASAKWA.




DAR ES SALAAM: Baadhi ya viongozi wa dini nchini wanadaiwa kukwepa kodi kwa kutumia taasisi zao za dini ambazo zimekuwa zikipata misamaha ya kodi kwa kile kinachoelezwa kuwa vitu wanavyoviingiza ni mali ya kanisa, misikiti au taasisi ya kidini, wakati baadhi yao hudanyanga, wanasakwa na serikali kwa kosa la kukwepa kulipa kodi.

Chanzo chetu cha habari ndani ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini zinasema kuwa viongozi hao wa kidini wamekuwa wakitumia mwanya huo wa misamaha ya kodi kujinufaisha wenyewe kwa kuingiza magari ya kifahari ambayo huyatumia wenyewe au wafanyabiashara wazoefu wa kukwepa kodi.

Akizungumza na Wikienda, afisa mmoja wa Takukuru jijini Dar ambaye aliomba hifadhi ya jina kwa kuwa siyo msemaji wa taasisi hiyo lakini alikiri kwamba kuna baadhi ya viongozi wa dini wanasakwa kutokana na madai ya kukwepa kodi kiujanja.

“Wamekuwa wakiingiza vitu vingi tu yakiwemo magari ya kifahari lakini hayatumiwi kwa shughuli za kidini badala yake wamekuwa wakitumia wenyewe katika shughuli binafsi au mengine yanaingizwa kwa jina la taasisi lakini utakuta ni mali zao au wafanyabiashara nje ya taasisi zao,” alisema afisa huyo.

Akaongeza: “Nakumbuka kuna viongozi fulani wa kidini walikamatwa na kuhojiwa katika ofisi zetu za Magomeni kwa kuingiza magari ya kifahari kumbe waliwaingizia watu kupitia taasisi yao ya kidini na huku wenyewe wakipanda daladala.”

Alisema viongozi hao waliyatoa magari hayo bandarini baada ya kupata msamaha wa kodi kupitia kwa mkuu wa wilaya lakini kuna taarifa kwamba sasa yanatembelewa na watu wenye fedha, hivyo uchunguzi wa suala hilo unaendelea.

Askofu mmoja wa Kanisa la Ufunuo Tanzania, Paul Bendera alikiri kusikia kuwa baadhi ya taasisi za kidini hutumia mali zinazoingizwa kwa jina la taasisi hizo lakini hutumika kwa matunizi binafsi na kuitaka serikali kuwachukulia hatua viongozi hao.

“Dini zote zinajenga amani ya nchi na kazi za serikali ni kuhakikisha kila mtu analipa kodi bila kujali dini au kabila. Serikali ichukue hatua za kisheria dhidi ya viongozi wa kidini wanaofanya hivyo,” alisema askofu huyo.

0 Responses to “VIONGOZI WA DINI WAKWEPA KODI WASAKWA.”

Post a Comment

More to Read