Tuesday, July 12, 2016
WAKIMBIZI WENYE UALBINO KUTENGEWA ENEO MAALUM KATIKA KAMBI YA NDUTA
Do you like this story?
Kambi ya wakimbizi ya
Nduta iliyopo wilayani Kibondo Mkoa wa Kigoma imewatengea eneo maalumu la
kuishi watu wenye ulemavu wa ngozi ili kulinda usalama wa maisha yao.
Hayo yamesemwa na
Mkuu wa Kambi hiyo, Peter Buluku alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii
juu ya maisha halisi ya wakimbizi hao wanaoishi katika kambi hiyo wakitokea
nchini Burundi.
Buluku amesema kuwa
katika kambi hiyo kuna baadhi ya wakimbizi wanaojihusisha na vitendo
vinavyohatarisha usalama wa wakimbizi wenzao vikiwemo vya ubakaji, wizi na
kujaribu kuteka watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mkuu huyo wa kambi
amefafanua kuwa mnamo mwezi Aprili mwaka huu, familia moja yenye mtoto mwenye
ulemavu wa ngozi ilivamiwa na watu wasiojulikana na kumchukua mtoto huyo lakini
kwa bahati nzuri majirani walijitahidi kupiga kelele hivyo,
watuhumiwa waliamua
kumtelekeza mtoto huyo na kukimbilia kusikojulikana.
“Kutokana na
kujitokeza kwa hali hiyo, Sisi pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali
yanayotoa huduma kambini hapa tuliamua kuwatengea eneo maalumu lililo karibu na
kituo cha polisi watu hawa wenye ulemavu wa ngozi ili wawe na ulinzi wa kutosha
hivyo kuishi kwa amani kama binadamu wengine”, alisema Buluku.
Hadi sasa kambi hiyo
ina jumla ya watu watano wenye ulemavu wa ngozi kutoka kwenye familia mbili
tofauti, Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR) limehaidi kujenga jengo
la kudumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu huo.
Kambi ya Nduta
ilianzishwa rasmi mwaka 1998 na kufungwa mwaka 2009. Ilifunguliwa kwa mara ya
pili mwaka 2015 baada ya kutokea kwa vurugu nchini Burundi na kusababisha
baadhi ya raia wa nchi hiyo kukimbilia nchini Tanzania, hadi sasa kambi hiyo
ina jumla ya wakimbizi 55,320 ambao ni raia wa Burundi.
Imeandikwa na
Jacquiline Mrisho – MAELEZO Kigoma
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WAKIMBIZI WENYE UALBINO KUTENGEWA ENEO MAALUM KATIKA KAMBI YA NDUTA”
Post a Comment