Monday, August 8, 2016
WAZIRI MKUU AIAGIZA WIZARA YA KILIMO,MIFUGO NA UVUVI KUWACHUKULIA HATUA WATENDAJI WOTE WALIOHUJUMU USHIRIKA
Do you like this story?
Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa mama mkulima jinsi ya kupata soko la alizeti.(Picha na David Nyembe wa Fahari News) |
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhakikisha
inafufua sekta ya ushirika na kuwachukulia hatua kali watendaji wote
waliohujumu ushirika na kusababisha machungu kwa wanaushirika ili iwe fundisho
kwa wengine.
Pia ameitaka
Wizara hiyo kupitia upya sekta ya ushirika kwa kuanza na viongozi walipo ndani
ya wizara hadi mikoani kuhakikisha kama wanafanya kazi zao ipasavyo na
kuwaondoa watakaobainika kwa uzembe.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo leo (Jumatatu, Agosti 08, 2016) wakati akifunga
maadhimisho ya sherehe za nane nane kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
yaliyofanyika kwenye uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya.
Hata hivyo
Waziri Mkuu amesema mkulima, mfugaji na mvuvi mdogo au mmoja mmoja hawezi
kupunguza umaskini bila ya kuwa na chombo cha kuwaunganisha na kuwapa nguvu ya
kutetea bei ya mazao yao kama ushirika. Aidha, ushirika imara utawasaidia
kutafuta soko, kupata mikopo ya riba nafuu.
Amesema
pamoja na umuhimu wa kuwepo kwa ushirika, tasnia hiyo imewaumiza wakulima wengi
na kuwafanya kukata tamaa katika uzalishaji kutokana na usimamizi mbovu,
ubadhirifu na ubabe wa baadhi ya viongozi wa ushirika.
“Wahimizeni
na kuwashawishi wakulima, wafugaji na wavuvi kujiunga katika vikundi vya
ushirika vya uzalishaji na SACCOS. Aidha, elimu ya ushirika inayotolewa kwenye
maonesho ya mwaka huu, iwe changamoto kwenu kwamba umoja ni nguvu na utengano
ni udhaifu,” amesema.
Wakati huo
huo Waziri Mkuu amesema Serikali haitamvumilia mfugaji anayelisha katika maeneo
ya hifadhi na vyanzo vya maji, Wakuu wa Mikoa na Wilaya waendelee kulinda
maeneo hayo.
Kwa upande
wake Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha alisema sekta ya
kilimo imekuwa na mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka mine
mfululizo nchi imeweza kuzalisha chakula cha ziada, ambapo kwa mwaka huu
imezalisha kwa asilimia 123.
“Mafanikio
hayo yanachangiwa jitihada za Serikali katika kutoa ruzuku ya pembejeo, taasisi
za utafiti ambazo zimekuwa zikitafiti aina bora ya mbegu zikitafuta mbegu bora
na wakulima walioamua kuwekeza kwenye kilimo,” alisema.
Naibu
Waziri Ole Nasha alisema katika ukanda wa Nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) ni nchi mbili tu za Tanzania na Zambia kati ya nchi 15 za
jumuia hiyo hazikabiliwiu na baa la njaa.
Licha ya
mafanikio hayo Naibu Waziri huyo aliwaomba wakulima kuendelea kuzalisha kwa
kufuata kanuni bora za kilimo pamoja na kutumia pembejeo bora.
Naye
Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini, Ladislaus Mwanakatwe ameipongeza Serikali kwa jitihada
zake za kuwatetea pamoja na utatuzi wa kero za muda mrefu zilizokuwa
zinawakabili wakulima ikiwemo ya tozo.
Hata hivyo
Mwanakatwe ameiomba serikali kuitafutia ufumbuzi changamoto ya upatikanaji wa
masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo. Pia ameomba Serikali iwezeshe Benki ya
Kilimo (TADB) kufungua matawi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ili wakulima
wake waweze kupata mikopo kwa urahisi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WAZIRI MKUU AIAGIZA WIZARA YA KILIMO,MIFUGO NA UVUVI KUWACHUKULIA HATUA WATENDAJI WOTE WALIOHUJUMU USHIRIKA”
Post a Comment