Sunday, November 13, 2016

MKUU WA POLISI AAGIZWA AANDAEJELA MAALUM YA WATUMISHI WATAKAOTUPWAJELA SAA 48




MKUU wa mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amemuagiza Mkuu wa Polisi, wilaya ya Sumbawanga, Mashenene Mayila kutenga chumba maalumu kwa ajili ya maofisa wa serikali na watendaji wa serikali za mitaa watakaoamriwa kukaa rumande kwa saa 48 wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao kwa uzembe, uvivu na ukaidi.

Akitoa maagizo hayo, Zelothe alionya kuwa hayuko tayari kuwavumilia watendaji wazembe, wavivu, wapiga ‘dili’ na walarushwa na kuongeza kuwa badala ya kuwatumbua atawapasua. Zelothe alitoa maagizo hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwa siku mbili mfululizo akikagua usafi katika stendi kuu ya mabasi iliyopo mjini Sumbawanga akisema kuwa inanuka kwa uvundo wa uchafu.

“Sitaki kusikia tena wala kushuhudia uchafu ukizagaa katika stendi hii kuu ya mabasi, stendi hii inanuka, serikali hii ya Awamu ya Tano haina ‘muhali’ sitamvumilia, mtendaji yeyote mzembe, mvivu, mkaidi na mla rushwa…nawaonya mie sitawatumbua bali nitawapasua. Namuagiza OCD wa Sumbawanga ahakikishe kituoni kwake anatenga chumba maalumu kwa ajili ya watendaji watakaoshindwa kutimiza majukumu yao kutokana na uzembe na uvivu,” alisisitiza.

Aidha aliamuru watendaji wanne wa manispaa ya Sumbawanga waliotupwa rumande na kulala huko usiku kucha wasimamie usafi wa stendi kuu ya mabasi mjini humo kabla ya kuachiwa huru.

Zelothe alipofanya ziara ya kushtukiza siku ya kwanza kwenye stendi hiyo kuu ya mabasi alikumbana na uchafu ukiwa umezagaa kila kona huku choo chake kikiwa kimefurika ambapo alimuagiza Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfani Haule kuwakamata na kuwaweka ndani maofisa wanne wa Manispaa ya Sumbawanga kwa saa 24, kwa kuacha choo cha stendi kuu ya mabasi kikiwa kimefurika.

Inaelezwa kuwa choo hicho kipo katikati ya mji na kimekuwa katika hali hiyo ya uchafu kwa muda mrefu, jambo ambalo linaweza kusababisha maradhi kwa watu wanaotumia maeneo ya karibu na choo hicho, wakiwemo wasafiri.

Maofisa watendaji hao ni Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Sumbawanga, Hamid Masare, Ofisa Mtendaji Kata ya Katandala, Charles Kalulunga, Ofisa Afya wa Kata ya Katandala, Edes Kakusa na Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Katandala, Maria Ntara.

Baada ya kusikiliza kero za watumiaji wa stendi hiyo kuu ya mabasi, Zelothe alimuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Sumbawanga Saad Mtabule ahakikishe uchafu uliorundikana katika stendi hiyo unazolewa usiku mpaka umalizike.

0 Responses to “ MKUU WA POLISI AAGIZWA AANDAEJELA MAALUM YA WATUMISHI WATAKAOTUPWAJELA SAA 48”

Post a Comment

More to Read