Sunday, November 20, 2016
NAIBU WAZIRI WA UJENZI ATUA MAKETE, ATOA TAMKO KUHUSU LAMI YA NJOMBE-MAKETE-MBEYA
Do you like this story?
Naibu Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amewataka wananchi
waliowekewa alama za kubomoa nyumba zao zilizopo pembezoni mwa barabara ya
Njombe-Makete hadi Mbeya KM 205 waanze kuhama kwenye nyumba hizo ili kupisha
zoezi la ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Akizungumza
mara baada ya kukagua barabara hiyo Eng. Ngonyani amesema awamu ya kwanza ya
ujenzi wake itaanza wakati wowote kuanzia sasa mara baada ya kupatikana
mkandarasi na mkandarasi mshauri ambayo itahusisha sehemu ya Njombe hadi Makete
KM 109.4.
“Kuweni
waadilifu waliowekewa alama za kijani kwenye nyumba zao watalipwa fidia lakini
wenye alama nyekundu hawatalipwa hivyo ni vizuri wote kutafuta maeneo mengine
ya makazi ili kuepuka usumbufu mara zoezi la ujenzi litakapoanza”. Amesema Eng.
Ngonyani.
Eng. Ngonyani
amesema kwa kuwa kazi ya ujenzi na ulipaji fidia zinagharamiwa na Serikali ni
vema zoezi la ujenzi wa barabara likaanza wakati Serikali ikitafuta fedha kwa
ajili ya fidia.“Ili tuweze kufanikiwa katika mambo yote tumeona tuanze na zoezi
lenye gharama kubwa ambalo ni ujenzi wa barabara kisha zoezi la fidia
litaendelea wakati ujenzi wa barabara unaendelea”. amesisitiza Eng. Ngonyani.
Naye Mkuu wa
Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi ameishukuru Serikali kwa jitihada za ujenzi
wa daraja la Ruhuhu linalounganisha Mkoa wa Njombe na Ruvuma na ameiomba
Serikali kuangalia namna ya kuweka lami barabara inayokwenda kwenye hospitali
ya Mkoa wa Njombe na ile inayoenda hospitali ya misheni ya Ikonda wilayani
Makete ili kuwezesha barabara hizo kupitika kwa urahisi wakati wote wa mwaka.
Katika hatua
nyingine Mbunge wa Makete Profesa, Norman Sigara amemuomba Naibu Waziri Eng.
Ngonyani kuhakikisha Mkandarasi anayejenga barabara ya Njombe –Makete na Makete
–Mbeya kupitia Kitulo anaanza kazi hiyo kwa wakati ili kuongeza kasi ya
wananchi kubomoa nyumba zao katika maeneo ya hifadhi ya barabara na hivyo
kuunganisha kirahisi mkoa wa Njombe na Mbeya kwa barabara ya lami.
Naibu Waziri
Ngonyani yupo katika ziara ya kukagua Miundombinu ya Barabara, Bandari na
Mawasiliano katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini ambapo tayari amekamilisha
ziara yake katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Ruvuma.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “NAIBU WAZIRI WA UJENZI ATUA MAKETE, ATOA TAMKO KUHUSU LAMI YA NJOMBE-MAKETE-MBEYA”
Post a Comment