Wednesday, November 16, 2016

WATOTO WAKUTWA PORI LA VIKINDU WAKIFUNDISHWA UGAIDI




Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia wanawake wanne na watoto wanne wanaofundishwa uhalifu wa kutumia silaha na mbinu za kigaidi katika kambi zilizomo kwenye misitu ya pori la Vikindu.

Kamishna wa Kanda hiyo, Simon Sirro amesema kikosi cha kupambana na uhalifu wa kutumia silaha na ujambazi cha kanda hiyo, kilifanya operesheni katika msitu huo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Kamanda Sirro ameeleza kuwa awali Polisi walipokea taarifa toka kwa mzazi wa kiume aliyefahamika kwa jina la Shaban Abdallah Maleck mkazi wa Kitunda kuwa ametoroshewa watoto wake wanne na mtalaka wake aitwaye Salma Mohamed anayetuhumiwa kuingizwa kwenye harakati za kigaidi.

Na kwamba baada ya taarifa hizo Polisi walianza kufanya msako katika misitu ya pori la Vikindu.
Amesema kuwa, baada ya watuhumiwa kuhojiwa imedhihirika kuwa watoto hao wameachishwa masomo na kuingizwa katika madrasa ambazo ndizo kambi walizokamatwa chini ya uangalizi wa wanawake.

Amesema watoto hao hufundishwa mbinu za mapigano, namna ya kutumia silaha pamoja na kufunzwa kupora au unyang’anyi kwa kutumia silaha.

Pia hufundishwa kujenga uadui na Polisi, walinzi katika taasisi za fedha, na makafiri.
Aidha, Kamanda Sirro amesema wanawake hao wanaendelea kufanyiwa mahojiano ili kuweza kubaini mtandao mzima ili kutokomeza tabia ya kufundisha watoto uhalifu hususani kwamba wanaochukuliwa ni wale wa kuanzia umri wa miaka minne na kuendelea.

0 Responses to “ WATOTO WAKUTWA PORI LA VIKINDU WAKIFUNDISHWA UGAIDI”

Post a Comment

More to Read