Sunday, March 19, 2017
AHADI TISA ZA MAKONDA 2016 ALIZOFUNGIA KABATINI
Do you like this story?
Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametekeleza mambo manane mapya ambayo hayakuwamo
kwenye orodha ya ahadi zake za mwaka jana wakati alipoingia madarakani.
Siku chache
baada ya kuapishwa, Makonda alikutana na wenyeviti wa Serikali za mtaa na
kuwaeleza mikakati tisa aliyopania kuifanya katika kulibadilisha Jiji la Dar es
Salaam.
Jumatano
iliyopita, Makonda aliadhimisha mwaka wake mmoja tangu ateuliwe kushika wadhifa
huo akielezea mambo 10 aliyoyafanya katika kipindi hicho na mengine 10
atakayoyafanya katika mwaka wake wa pili.
Wachambuzi
wa masuala ya sayansi ya siasa wamempongeza kiongozi huyo na kusema hata kama
hajatimiza baadhi ya ahadi, lakini amekuwa mbunifu kwa kujifanyia tathmini
ukilinganisha na viongozi wengine.
Mipango
aliyotekeleza
Mambo
aliyotekeleza ambayo hayakuwamo kwenye orodha ya mikakati yake ni kampeni ya
mti wangu, ujenzi wa wodi ya wagonjwa, vita ya dawa za kulevya, ujenzi wa ofisi
ya Bakwata, kampeni ya uchangiaji wa damu, marufuku ya shisha na migogoro ya
ardhi.
Ahadi tisa
za 2016
Wakati
alipoingia madarakani na kuzungumza na wenyeviti wa Serikali za mtaa, Makonda
aliahidi usafi wa jiji, ofisi za Serikali kutokuwa za chama, kutenga maeneo ya
biashara, sensa ya nyumba kwa nyumba, usalama wa raia na mali zao, watumishi
hewa, kurudisha hadhi ya watendaji wa Serikali za mitaa, elimu na barabara.
Kwenye suala
la usafi, Makonda aliahidi zawadi ya gari la Sh20 milioni au fedha taslimu kwa
mwenyekiti ambaye mtaa wake utaongoza kwa usafi na Sh5 milioni kwa kila mjumbe
wa mtaa husika. Pia, alisema zawadi hiyo itakayokuwa ikitolewa kila baada ya
miezi mitatu na kwamba ingeanza Aprili Mosi, 2016.
Licha ya
kusema kuwa amefanikiwa kufanya mambo kumi, Makonda ameshindwa kutekeleza ahadi
tisa za mwaka jana alizoahidi mwaka jana.
Kuhusu
usalama
Mwaka jana,
Makonda aliahidi kutoa pikipiki 30 kwa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam
ili kuwawezesha askari kuwafuatilia watu watakaotupa taka ovyo barabarani.
Kwenye suala
la usalama wa raia na mali zao, kiongozi huyo alisema kila mwenyekiti wa mtaa
anapaswa kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama na hilo litafanikiwa endapo
atakuwa na utaratibu wa kujua nani anafanya nini.
Ofisi za
Serikali
Suala la
ofisi za Serikali kuwa za chama, mkuu huyo wa mkoa alisema ofisi za Serikali ni
kwa ajili ya kazi na siyo sehemu ya kufanyia siasa akisema katika uongozi wake
haangalii chama, bali kusikiliza matatizo ya kila mtu.
Kutenga
maeneo ya biashara
Katika
kutenga maeneo ya biashara, Makonda alisema matamanio yake ni kuiona Dar es
Salaam ya kisasa ambayo itakuwa na maeneo maalumu kwa ajili ya biashara ya
vileo, magari, gereji na vifaa vya ujenzi.
Aliwaagiza
wakurugenzi wa manispaa ifikapo Mei Mosi wawe wameainisha maeneo maalumu kwa
ajili ya biashara hizo.
Barabara za
biashara
Makonda
aliahidi kuzungumza na wakurugenzi wa manispaa ili kuangalia namna ya kuandaa
utaratibu wa kutenga barabara moja kwa kila kata kwa siku moja ili watu wafanye
biashara.
Sensa ya
wakazi wa Dar
Katika suala
la sensa nyumba kwa nyumba aliwataka wenyeviti wa mitaa kupita kila nyumba
katika mitaa yao kuorodhesha idadi ya watu wanaoishi na shughuli zao.
Alisema hiyo
itasaidia pia kujua watu wasiokuwa na ajira hivyo kujipanga namna ya
kuwasaidia.
Ahadi kwa
polisi
Aliahidi
kutoa Sh1 milioni kwa polisi atakayepambana na majambazi, huku milioni moja
nyingine ikienda kwa mtu atakayesalimisha bunduki au bastola kituo cha polisi.
Watumishi
hewa
Akizungumzia
watumishi hewa, alitoa agizo: “Nitakapoagiza orodha ya watumishi hewa ije
kamili, kinyume na hapo ofisa utumishi atalazimika kulipa hata madeni
yaliyopita maana anaonekana ana nia ya dhati ya kufuga uozo huo.”
Ofisi za
watendaji wa mitaa
Makonda pia
aliwaahidi kuwajengea ofisi wenyeviti wote wa Serikali za mitaa na kuachana na
habari za kupanga na kwamba, ifikapo Aprili Mosi atawakopesha pikipiki 1,000
ili ziwasaidie katika utendaji wao wa kazi na kuwasaidia kujikimu kimaisha.
Barabara
Kuhusu kero
ya barabara, aliahidi kuzishughulikia, huku akiwashangaa wahandisi kwa kukaa
ofisini.
Mafanikio 10
aliyotaja
Baada ya
mwaka mmoja, mkuu huyo wa mkoa alibainisha mambo aliyoyafanya ndani ya mwaka
huo mmoja.
Aliyataja
mambo hayo kuwa ni kuendesha kampeni ya mti wangu inayohamasisha upandaji miti,
ujenzi wa wodi za wagonjwa, vita dhidi ya dawa za kulevya na kutatua migogoro
ya ardhi kwa wananchi.
Mambo
mengine aliyoyafanya ni ujenzi wa Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu
Tanzania (Bakwata), kampeni ya kuchangia damu, utengenezaji wa madawati kwa ajili
ya shule za umma, uhakiki wa silaha, usafi wa jiji na kupiga marufuku matumizi
ya shisha.
Ahadi mpya
10 alizotoa
Makonda
alibainisha pia mambo mengine 10 atakayoyafanya katika mwaka wake wa pili wa
uongozi akianza na kusimamia watumishi wa umma kutekeleza wajibu wao katika
ngazi ya Serikali za mitaa mpaka ya mkoa.
“Nitapita
kuanzia ngazi ya Serikali za mtaa na kila mtendaji atanieleza namna
anavyowahudumia wananchi. Wananchi wanakuja mpaka ofisi ya mkuu wa mkoa kuleta
kero zao wakati zinaweza kutatuliwa kwenye mitaa yao, hatuwezi kwenda namna
hiyo,” alisema.
Makonda
ambaye amejipatia umaarufu zaidi kutokana na vita dhidi ya dawa za kulevya,
alisema atahakikisha kwamba anawahudumia waathirika wa dawa hizo kwa kuwapatia
tiba ya uraibu wao.
Kuhusu
wakazi wa mabondeni, alisema atahakikisha wote wanaoishi katika maeneo hayo
wanahama na tayari ameagiza nyumba zao kubomolewa kwa ajili ya kulinda usalama
wao.
Alisema
wakazi waliopewa viwanja katika maeneo hayo ambao wana hati za viwanja hivyo,
atawapatia ardhi sehemu nyingine kwa sababu ni uzembe wa watendaji wa Serikali
na kusisitiza kwamba watakaobainika kuhusika na uzembe huo watawajibishwa.
Asifiwa wa
wasomi
Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema hadi hapo Makonda
ameonyesha ushujaa kwa kuwa mkuu wa mkoa wa kwanza kuelezea utekelezaji wa
ahadi zake. “Ingekuwa ni kugawa medali kijana huyu angepata licha ya
makandokando yanayomzunguka, amefanya kazi nzuri, amethubutu na ni mbunifu,”
alisema.
Alisema
kwenye utendaji wa kazi jijini Dar es Salaam, kiongozi huyo wa mkoa anasikika
zaidi katika uchapaji wa kazi kuliko viongozi wa kuchaguliwa wakiwamo wabunge
na mameya.
Hata hivyo
alisema ni wakati wa viongozi wengine kujitathmini na kuelezea yale
waliyoyafanya.
Kuhusu ahadi
ambazo hajazitekeleza, Dk Bana alisema muda bado na kwamba, ikiwa atadumu
kwenye nafasi hiyo huenda utekelezaji wa ahadi zake ungekuwa juu zaidi.
Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema mara nyingi viongozi huwa
wanatekeleza mipango ambayo haikuwepo kwenye ratiba zao kutokana na kuibuka
ghafla au umuhimu wake.
Alisema ni
afadhali Makonda kwa kuwa ameonyesha kwa vitendo hata kama hakutimiza ahadi
zake za awamu iliyopita kuliko, kukaa kimya bila kujifanyia tathmini ulikofanikiwa
na kushindwa.
“Hatua ya
kujifanyia tathmini naweza kusema ni ya kishujaa, wakuu wa mikoa wengine
wanaweza kuiga hii itawafanya watimize yale wanayoyapanga na hivyo kuwaletea
wananchi maendeleo,”alisema.
Mchambuzi wa
uchumi mkoani Arusha, Dk Godwin Maimu alisema hatua ya kiongozi huyo
kujitathmini ni nzuri japo anapaswa, kutekeleza ahadi zake kwa wananchi licha
ya kuwa si kiongozi wa kuchaguliwa.
“Bado jiji
la Dar es Salaam linakabiliwa na tatizo la wamachinga kutengewa maeneo kwa
ajili ya biashara, amejitahidi lakini lazima awe na vipaumbele kwa masuala ya
msingi anayodhani atayatekeleza,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “AHADI TISA ZA MAKONDA 2016 ALIZOFUNGIA KABATINI”
Post a Comment