Sunday, March 19, 2017
MBIO UBUNGE AFRIKA MASHARIKI ZAANZA
Do you like this story?
Baada ya
Ofisi ya Bunge kutangaza kuwa Aprili 4 ni siku ya uchaguzi wa wajumbe tisa wa
Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kutoka Tanzania, vyama vya siasa vimeanza
mchakato wa uteuzi.
Tayari vyama
vya Chadema na CCM vimeshatoa masharti ya kuwania nafasi hiyo ikiwamo ada
itakayotozwa.
Ofisi ya
Bunge juzi ilitoa taarifa kuwa wenye nia ya kuwania nafasi hiyo watangaze
kupitia kwenye vyama vyao vya siasa.
Wajumbe wapya
watachukua nafasi zinazoachwa wazi na Makongoro Nyerere, Shy-Rrose Bhanji,
Bernard Murunya, Adam Kimbisa, Abdulla Mwinyi, Mariam Yahya Ussi, Angela
Kizigha, Twaha Taslima na Nderakindo Kessy.
Bunge
kupitia taarifa yake hiyo ilisema uteuzi utafanyika Machi 30 na uchaguzi
utafanyika baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Taarifa
iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Tumaini
Makene ilieleza mchakato ndani ya chama hicho umefunguliwa na uteuzi utafanyika
Machi 22.
“Wanachama
wote wenye sifa na vigezo vya kuwania nafasi hiyo kupitia Chadema wanatakiwa
kuchukua na kujaza fomu za kuomba uteuzi huo,” alisema Makene.
Alisema
vituo ambako fomu hizo zitapatikana ni ofisi za makao makuu ya chama hicho Mtaa
wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam na ofisi zote za kanda 10 za Chadema
Tanzania Bara na Zanzibar na ofisi za mikoa na majimbo.
Makene
katika taarifa hiyo alisema mwanachama atakayechukua fomu anatakiwa
kuambatanisha stakabadhi ya malipo ya ada ya Sh500,000 na wasifu wake, nakala
ya cheti cha kuzaliwa au hati ya kusafiria.
Pia,
anatakiwa kuwa na nakala ya kadi ya uanachama na kuwa na sifa za kugombea kama
zilivyoainishwa kwenye ibara ya 67 ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977.
Wakati
huohuo, CCM katika taarifa yake iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi,
Humphrey Polepole jana ilisema imepokea mwaliko kutoka kwa Katibu wa Bunge na
fomu zitaanza kutolewa leo na mwisho wa kuzirejesha ni Machi 23 saa 10:00
jioni.
Wakati ada
ya fomu kwa Chadema ikiwa Sh500,000, CCM imesema zitatolewa kwa wanachama wake
kwa ada ya Sh100,000.
Polepole
alisema fomu zitatolewa makao makuu ya CCM Dodoma, ofisi ndogo za makao makuu
Zanzibar na Lumumba, Dar es Salaam.
Taarifa hiyo
ilisema chama hicho hakitasita kuwachukulia hatua ikiwamo kuwafutia sifa ya
uteuzi wagombea watakaokiuka katiba ya CCM, kanuni za uchaguzi na kanuni za
uongozi.
Alisema,
“Inasisitizwa katika muktadha na uhalisia wa mageuzi makubwa ya chama chetu
ambayo yanalenga kutupatia aina ya viongozi waadilifu, waaminifu, wachapa kazi,
wawajibikaji, wanaochukizwa na rushwa na wanaoweka maslahi ya chama na nchi
mbele.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MBIO UBUNGE AFRIKA MASHARIKI ZAANZA”
Post a Comment