Thursday, March 9, 2017

MFANYABISHARA AJIPIGA RISASI BAADA YA KUKUTWA NA SHEHENA YA VIROBA


 
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, amethibitisha tukio la kujiua kwa wakala wa uagizaji na usambazaji wa vinywaji mbalimbali ikiwemo pombe za vifungashio aina ya viroba, Festo Mselia.
Mfanyabiashara huyo ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Mselia Enterprises anadaiwa kujiua kwa kujipiga risasi chini ya kidevu shambani kwake eneo la Msalato, nje kidogo ya mji wa Dodoma, baada ya polisi kumbaini akiwa amehifadhi shehena ya viroba, pombe ambazo serikali imepiga marufuku matumizi yake.
Akizungumzia tukio hilo  Kamanda Mambosasa alisema kabla ya kujiua, mfanyabiashara huyo aliitwa kwa mahojiano polisi na kisha uamuzi ulifanyika kwamba shehena ya viroba aliyokutwa nayo katoni 1,269 isiuzwe. Hata hivyo, kamanda huyo amesisitiza kwamba taarifa zaidi zitatolewa baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika.
Lakini katika hatua nyingine, mmoja wa wanafamilia amezungumzia tukio hilo akidai siku ya Ijumaa (Machi 3, 2017) polisi walifika katika duka lake lililopo barabara ya 11 na kumtaka mmiliki wa duka hilo kufika Kituo Kikuu cha Polisi siku ya Jumatatu (6/3/2017), alifanya hivyo na kisha kurudi kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
Mwanafamilia huyo (jina linahifadhiwa) alidai kuwa asubuhi ya jana (7/3/2017) mke wa mfanyabiashara huyo alikwenda shambani na majira ya saa za mchana alirudi dukani baada ya mumewe kumtaka kufanya hivyo.
“Ilipofika majira ya saa 10 jioni gari mbili za polisi ikiwemo ya Kamanda wa Polisi Dodoma ziliegeshwa dukani hapo huku Mselia akiwa kwenye gari yake aina ya Prado akiendeshwa na rafiki yake aliyejulikana kwa jina moja la Mazengo.
“Aliposhuka kwenye gari alionekana kutokuwa katika hali ya kawaida,  waliingia ndani dukani pamoja na polisi na baada ya muda mfupi walitoka na kuondoka,” alidai
Kwa mujibu wa mwanafamilia huyo ilipofika majira ya jioni alipiga simu ya marehemu bila majibu hivyo alijua ametangulia nyumbani, lakini baadaye alipigiwa simu na mtu mwingine akimueleza kuwa amepigiwa simu na polisi kuwa kuna mfanyabiashara amejiumiza shambani kwake.
Kwa upande wake, kijana wa shamba aliyejitambulisha kwa jina la Baraka John alidai kuwa majira ya saa 12.30 jana (Machi 7, 2017) jioni alirejea nyumbani kutoka kulisha mifugo na kumkuta Mazengo akiwa amekaa kwenye mti.
“Mazengo ambaye ni mgeni kwangu aliniambia ameachwa hapo na Mselia ambaye ameenda shamba na kunieleza nichukue baiskeli na kumfuatilia huko shamba kwani ni muda mrefu umepita tangu aondoke,” alidai na kuongeza kuwa alipofika hilp alimkuta anatapata, hali iliyomlazimu kurudi kuomba msaada kwa Mazengo na majirani zake.
Naye Afisa Mtendaji Kata ya Msalato, Herman Malindila, alidai kuwa majira ya saa moja na nusu usiku wa jana alipokea taarifa kutoka kwa mtu aliyejiita mama Mboya akimtaarifu kuwa kulikuwa na mtu kajipiga risasi shambani.
Alifika eneo la tukio na kukuta wananchi huku kukiwa na ‘muungurumo’ wa mtu akiugulia maumivu huku pembeni yake kukiwa na bastola hivyo kuchukua uamuzi wa kuwaita polisi ili wafike eneo la tukio.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, James Charles, amethibisha kifo cha mfanyabiashara huyo akidai kuwa alipokelewa majira ya saa mbili usiku kama majeruhi na kujitahidi kumpa huduma ya kwanza lakini ilipofika majira ya saa tano usiku wa kuamkia leo (Machi 8, 2017) alifariki dunia.

0 Responses to “MFANYABISHARA AJIPIGA RISASI BAADA YA KUKUTWA NA SHEHENA YA VIROBA”

Post a Comment

More to Read