Thursday, March 9, 2017

USHIRIKI WA WANAWAKE SERIKALINI WATAJWA KUWA NI 20%


Ikiwa Machi 8, 2017, ni maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani, Mashirika yanayotetea haki za wanawake nchini yameendelea kuisisitiza serikali kuongeza juhudi za kumlinda mwanamke na haki zake za msingi. Kwa kuboresha sheria, sera, na mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ambayo imelenga kumwinua mwanamke kiuchumi, kijamii na kisisasa.
Mashirika hayo ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), na Kituo cha Msaada kwa Wanawake (WLAC).
Wakati akisoma tamko la mashirika hayo jijini Dar es Salaam, katika hafla za maadhimisho ya siku ya wanawake yaliyobeba kaulimbiu ya ‘Tanzania ya viwanda, wanawake ni msingi wa mabadiliko kiuchumi’ .
Naemy Sillayo amesema kuwa, licha ya serikali kuonyesha jitihada za kuleta usawa baina ya wanaume na wanawake bado kuna ombwe la usawa katika upatikanaji wa fursa ukilinganisha na wingi wao ambapo kwa mujibu wa takwimu ya sensa ya mwaka 2012 inaonyesha idadi ya wanawake nchini ni asilimia 51 wakati wanaume ikiwa 49%.
Sillayo ameeleza kuwa,  bado serikali haijafanikiwa kutoa fursa sawa ya ushiriki wa wanawake katika uongozi, na kufafanua kwamba wanawake walioko bungeni ni 30%, wakati katika baraza la mawaziri likiwa na wanawake 4 kati ya mawaziri 19, hali kadhalika katika wilaya 134 wanawake wamepewa nafasi 25, huku katika ukurugenzi wa halmashauri wanawake wakipewa nafasi 33 kati ya 185. Vile vile kwa upande wa wakuu wa mikoa wanawake walioteuliwa ni 4 kati ya 26.
Amesema kufuatia idadi hiyo, serikali bado haijafanikiwa kuleta usawa wa asilimia 50 katika ushiriki wa uongozi kwa kuwa hali ya ushiriki wa wanawake iliyopo sasa ni sawa na asilimia 20.

0 Responses to “USHIRIKI WA WANAWAKE SERIKALINI WATAJWA KUWA NI 20%”

Post a Comment

More to Read