Wednesday, April 5, 2017
HUKU SAKATA LA MCHANGA WENYE MADINI LIKIUNDIWA TUME,MKEMIA WA MADINI BONGO ATEKWA
Do you like this story?
Na WAANDISHI WA| GAZETI LA UWAZI| HABARI
MWANZA: Habari kubwa inayotikisa nchi kwa sasa ni ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kuzuia mchanga wenye madini kwenye makontena bandarini Dar kupelekwa nje ya nchi na ameunda tume ya kufuatilia, lakini habari ya kushangaza ni Mkemia wa Madini wa Kampuni ya SGS ya jijini hapa, Yusuf Kapanda (48), mkazi wa Nyakato, ametekwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wa kundi la maharamia na kutishia kumuua kama wasipopewa dola za Kimarekani milioni 5 (sawa na shilingi bilioni 10 za Kitanzania).
Tukio hilo la kutisha lilitokea Machi Mosi, mwaka huu kwenye Mgodi wa Namoya ulioko Jimbo la Maniema, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ‘DRC’ ambapo imeelezwa kuwa watekaji walikuwa wamevaa kininja ili wasijulikane huku wakiwa na silaha nzito za kivita.
ALITEKWA NA WENGINE WATANO
Kwa mujibu wa mkewe, Mariam Dafi, Kapanda, akiwa na wenzake watano, akiwemo mmoja raia wa Kongo, watatu wa kutoka nje ya Bara la Afrika, walitekwa na kundi hilo na kupelekwa sehemu isiyofahamika huku watekaji wakipiga simu na kutaka fidia ya dola milioni 5 ili kuwaachia huru.
MKE WA KAPANDA AZUNGUMZA NA UWAZI
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Uwazi lilizungumza na ndugu wa Kapanda, akiwemo mkewe mwenye watoto wanne ambaye amejawa na simanzi kufuatia tukio la kutekwa kwa mumewe.
“Mume wangu ni mfanyakazi wa Kampuni ya SGS ya hapa Mwanza lakini makao yake makuu yapo Dar. Yeye ni mkemia wa madini. Na SGS ndiyo iliyompeleka kule Congo kufanya kazi ya mkataba na Kampuni ya Banro Corperation.
“Nilikuwa na tabia ya kuwasiliana naye kila baada ya siku mbili, lakini kuna siku nilishangaa kuona kuwa hapatikani hewani kwenye simu yake, nilivumilia nikiamini nitampata baadaye.”
TAARIFA YA KUTEKWA YAFIKA NYUMBANI
“Siku hiyo, bosi wake mmoja kutoka SGS alikuja nyumbani na kuniambia kuwa, mume wangu ametekwa Congo na wao kama kampuni wanafuatilia suala hilo kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Congo.
“Kusema kweli nilishtuka sana na pia nilishangaa. Mume wangu ametekwa!! Niliuliza hali yake, nikaambiwa yupo salama ila watekaji wametaka kiasi hicho cha pesa. Niliwaambia watoto hali halisi, nyumba ikawa kama ina msiba. Basi, nilimwachia Mungu na kumuombea mume wangu.”
MKE ASIMULIA MAZITO YA MUMEWE
“Kuna siku watekaji walimpa simu mume wangu, akanipigia, niliongea naye, akanimbia kuwa, nimlindie watoto na baba yake mzazi kwa sababu kule aliko yuko kwenye hatari ya kufanyiwa lolote lile. Kauli ambayo nikiikumbuka inaniumiza sana moyoni wangu.”
WAOMBA DOLA ELFU 20
“Siku nyingine, watekaji wakaanza kunipigia simu mimi wao wenyewe moja kwa moja na kuniambia niwatumie dola elfu ishirini (20,000) ili wamuachie mume wangu la sivyo watamfanyia kitu kibaya, niliwaambia kwa upole kuwa, natafuta hiyo pesa, wakakata simu.”
WASHUSHA DAU
“Kesho yake tena, walinipigia simu na kuniambia kuwa, niwatumie dola elfu kumi (10,000) wamuachie mume wangu, bado nikawaambia kwa upole, ndiyo natafuta.”
MKE APIGIWA SIMU ZA MFULULIZO
“Ilifika mahali sasa, kila siku wale watekaji wakawa wananipigia simu zaidi ya mara ishirini kwa muda wa wiki mbili mfululizo wakinitisha kuwa, niwatumie fedha la sivyo wanamdhuru mume wangu, nikijaribu kuwauliza maswali wanakata simu.”
ASHINDWA KULALA SIKU TANO
“Kutokana na simu za fujo za mfululizo kila baada ya nusu saa au saa moja, ilifika wakati nikashindwa kulala kwa muda wa siku tano. Kwani ilikuwa simu simu, kila muda simu.”
WAKO KATIKATI YA BONDE PORINI
“Ile siku nilipoongea na mume wangu, aliniambia wako porini lakini kwenye bonde, hivyo wakitaka kupiga simu wanapandishwa juu ya mlima ndipo wanawasiliana na mimi. Kwa kweli hili tukio linaniumiza sana.”
ATOA TAARIFA POLISI
“Siku ileile nilipopewa taarifa, nilikwenda kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza (Sentro) ambapo niliambiwa kuwa, Kampuni ya SGS ndiyo inatakiwa kwenda kutoa taarifa wakasema hata hivyo, masuala ya nchi na nchi hushughulikiwa na ubalozi.”
MUME ALIPANGA KUACHA KAZI
“Kusema ukweli, mume wangu alikuwa akifanya kazi katika mazingira magumu mno kule Namoya kwani ni porini sana. Aliwahi kuniambia kwamba, akirudi Tanzania ataomba kuhamishiwa sehemu nyingine ya kazi lakini si Namoya na kama ikishindikana basi angepumzika kazi.”
UWAZI LAIFIKIA NAMOYA
Kupitia teknolojia za kisasa za mawasiliano, Uwazi lilifanikiwa kuzungumza na mmoja wa wafanyakazi wa Mgodi wa Namoya nchini Congo ambaye hakuwa tayari kutoa ushirikiano wa aina yoyote zaidi ya kusema yeye hana mamlaka ya kuzungumza, labda gazeti lifike ofisi za SGS nchini Tanzania.
UWAZI LATINGA SGS
Uwazi lilifika makao makuu ya SGS yaliyopo Mtaa wa Mafinga, Kinondoni jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuzungumza na mmoja wa wafanyakazi ambaye aliliambia Uwazi liombe ‘apointimenti’ ya kuonana na ofisa utumishi, lakini hakutoa njia za kumpata ofisa huyo.
BOSI WA SGS MWANZA
Hata hivyo, Uwazi lilifanikiwa kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa SGS jijini mwanza aliyefahamika kwa jina moja la Kiki ambaye alisema yeye hana cha kuzungumza zaidi na kulitaka gazeti kuwasiliana na Balozi wa Tanzania nchini Congo.
“Nani kakuambia uwasiliane na mimi? Wasiliana na Balozi wa Tanzania Congo,” alisema Kiki kwa lugha ya Kiingereza ‘yai.’ Simu ya ubalozi wa Tanzania nchini Congo iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
WIZARA YA MAMBO YA NJE
Ijumaa na Jumamosi iliyopita, gazeti hili lilikwenda mbele zaidi kwa kumtafuta Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga ambaye simu yake iliita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi hakujibu.
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
Mchana wa Jumamosi iliyopita, Uwazi lilimpigia simu, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Injinia Hamad Masauni ili kumsikia ana lipi kuhusu tukio hilo, akasema:
“Aaa! Yule bwana Kapanda? Hebu nipigie jioni sana tuongee.” Jioni, naibu waziri huyo hakuwa hewani, Jumapili asubuhi alipokea na kusema:
“Hiyo ishu bwana, mpigieni waziri mwenyewe (Mwigulu Nchemba) lakini asipopatikana rudi kwangu tuongee.” Waziri Nchemba hakupatikana hewani, ikabidi Uwazi limrudie Naibu Waziri Masauni ambaye sasa hakupokea simu kabisa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “HUKU SAKATA LA MCHANGA WENYE MADINI LIKIUNDIWA TUME,MKEMIA WA MADINI BONGO ATEKWA”
Post a Comment