Wednesday, April 5, 2017
BASI LA LEO LAPATA AJALI ,ABIRIA 48 WANUSURIKA KIFO
Do you like this story?
WATU wanane wamejeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Leo Luxury walilokuwa wakisafiria kutoka Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara kwenda jijini Dar es Salaam kupinduka. Majeruhi hao wanane ambao walikuwa ni miongoni mwa abiria 48 wa basi hilo, wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Lindi ya Sokoine kwa matibabu.
Habari zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi na Idara ya Afya Mkoa zilieleza kuwa ajali hiyo ilitokea eneo la Mambulu Kata ya Mbanja Manispaa ya Lindi juzi saa 6:15 mchana.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Emmanuel Bomani, pia alithibitisha kupokea majeruhi 19 ambao kati yao, 11 walitibiwa na kuruhusiwa kuendelea na safari huku wanane wakibaki hospitalini hapo kuendelea na matibabu.
Dk. Bomani aliwataja waliolazwa hospitalini hapo kuwa ni pamoja na kondakta wa basi hilo, Hassan Ally, mkazi wa Kurasini jijini Dar es Salaam, Fatuma Mohamed, mkazi wa Mji Mkongwe wa Kivinje wilayani Kilwa, Fatuma Ndimba, mkazi wa Newala mkoani Mtwara, Shariff Mpanga, mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam, Joseph Mazengo, mkazi wa Ng’alizo mkoani Dodoma, Shaibu Mdimba, mkazi wa Newala mkoani Mtwara, Peter Kamandu, mkazi wa Chamwino mkoani Dodoma na Mwinyi Seif, mkazi wa Mwandege mkoani Pwani.
“Majeruhi wawili kati ya hao wanane waliolazwa, kondakta Hassan na abiria Fatuma Mohamed, bado hali zao siyo nzuri lakini wengine sita hali zao zinaendelea vizuri,” alisema Dk. Bomani.
Baadhi ya majeruhi hao, Shariff Mpanga, alidai kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi kutokana na kufukuzana na basi la kampuni ya Buti la Zungu lililokuwa mbele yao.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Lindi, Mohamed Likwata, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa ilihusisha basi lenye namba za usajili T 471 DDW, likiendeshwa na Ally Kaniki, mkazi wa Kibamba jijini Dar es Salaam.
Kamanda Likwata alisema dereva wa basi hilo anashikiliwa polisi kwa mahojiano kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
Aidha, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi huku akiwaonya madereva kuwa makini wakati wote.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BASI LA LEO LAPATA AJALI ,ABIRIA 48 WANUSURIKA KIFO”
Post a Comment