Tuesday, February 25, 2014

WATU WANAOSADIKIKA KUWA NI MAJAMBAZI WAFUNGA BARABARA MBEYA/NJOMBE WAPORA MALI NA KUJERUHI


Kamanda wa mkoa mbeya Ahmed  Msangi (Picha na Maktaba)


Na David Nyembe ,Mbeya.

POLISI Mkoani Mbeya, inawashikilia watu 10 wanaosadikiwa ni majambazi kwa tuhuma za kushusika na ufungaji wa  barabara kuu ya Mbeya/Njombe na kufanikiwa kupora mali za abiria waliokuwa wakisafiri na kujeruhi watatu.


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Robert Mayala, amesema tukio hilo limetokea February 24 mwaka huu majira ya saa saba za usiku katika Kijiji cha Machimbo Tarafa ya Rujewa wilayani Mbarali.

Amesema,watu hao wakiwa na silaha za jadi, mapanga, marungu, mawe na fimbo waliweka mawe makubwa na magogo kwenye barabara hiyo na kuteka baadhi ya magari yaliyokuwa yakipita.

Amesema, baadhi ya abiria waliporwa fedha taslimu, simu za mkononi na mikoba ambayo thamani na idadi bado haijafahamika huku abiria watatu wakijeruhiwa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za miili yao kwa kutumia silaha za jadi.



Mbali na kujeruhi na kuiba vitu mbalimbali pia wahalifu hawa wamefanya uharibifu katika baadhi ya magari kwa kuvunja vioo ikiwa ni pamoja na gari lenye namba za usajili T.867 ARX aina ya Toyota Noah lililokuwa likiendeshwa na dereva Ahmed Abdalah,” amesema Mayala.


Hata hivyo, amesema Askari waliokuwa doria  kutoka Mkoa wa Mbeya na Njombe walifanikiwa kufika kwa wakati kwenye eneo la tukio  na kukuta magari yakiwemo yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi(IT) yakiwa yamesimamishwa na kwamba watu hao walipoona  gari la polisi walikimbilia vichakani na magari kuendelea na safari zake.
Mwisho.

0 Responses to “WATU WANAOSADIKIKA KUWA NI MAJAMBAZI WAFUNGA BARABARA MBEYA/NJOMBE WAPORA MALI NA KUJERUHI”

Post a Comment

More to Read