Monday, March 3, 2014

WAFANYAKAZI KUANDAMANA KUPINGA POSHO KWA WABUNGE.


MAANDAMANO YA WAFANYAKAZI

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Dodoma limesema iwapo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wataongezwa posho, watafanya maandamano ya amani nchi nzima.

Pia maandamano hayo yatatumika kuwasilisha madai ya wafanyakazi wanaoidai Serikali kutokana na malimbikizo ambayo wameshindwa kulipwa.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa TUCTA wa Mkoa wa Dodoma, Dk Kamudu Ndenge, wakati akitoa tamko la viongozi wa vyama vya wafanyakazi Dodoma kwa vyombo vya habari kuhusu madai ya malipo wanayolipwa wabunge hao.  

Alisema watashangaa ombi lao likikubaliwa na kuongezwa posho wakati kuna wahudumu wa idara mbalimbali ambako wafanyakazi wanapokea mishahara ya Sh 150,000 kwa mwezi.

"Rais (Jakaya Kikwete) asikubali kuongeza posho hiyo maana tumeshuhudia hadi muda huu Serikali ikishindwa kulipa madai ya wafanyakazi kwa maelezo ya kutokuwa na fedha," alisema.

Dk Ndenge alisema kimsingi hawapingi nia yao ya kulalamika na kutaka kuongezwa posho kutoka Sh 300,000 wanayolipwa sasa kwa sababu ni haki yao ya kikatiba zifike Sh 500,000 kiasi ambacho wanaamini kitawafaa katika kutatua matatizo yao ya msingi wakiwa  Dodoma.

"Lakini tukiwa wote ni Watanzania tujiulize maswali, je kuna kiwango cha posho kinacholingana na Sh 300,000 kinacholipwa kwa watumishi wa Serikali wengi kwa mujibu wa nyaraka za Serikali wanaposafiri kikazi kuja hapa Dodoma ambako kuna maisha magumu?" Alihoji.

Aliendelea: “Ni kweli wakati wa Bunge viwango vya posho kwa watumishi wanaohudhuria vikao vya Bunge kutoka maeneo mbalimbali  hubadilishwa na kulipwa Sh 300,000 au zaidi kwa sababu ya gharama kubwa za maisha?"

Alisema kama majibu ni hapana kwa maswali hayo kwa nini wajumbe wa Bunge la Katiba waone maisha ni magumu wakati kuna baadhi ya watu wanaoshiriki kikao hicho na wako katika ngazi za uamuzi lakini hawajathubutu kuwafikiria kuwaongezea posho.


0 Responses to “WAFANYAKAZI KUANDAMANA KUPINGA POSHO KWA WABUNGE.”

Post a Comment

More to Read