Tuesday, April 8, 2014

MBWA WALIOMLA MTOTO NA KUSABABISHA KIFO CHAKE NUSURA WAMLE BABA MTU.




ZIMEKATIKA wiki mbili tangu kuzikwa kwa mtoto Christian Alex (6)  aliyeuawa kwa kushambuliwa na mbwa watatu waliodaiwa ni wa Ubalozi wa Qatar nchini, mbwa hao wamemkosakosa baba mtu.

Tukio la kuuawa kwa mtoto huyo lilijiri Kunduchi  Jangwani Beach jijini Dar Machi  26, mwaka huu.

Kwa mujibu wa chanzo, mara baada ya kumaliza shughuli ya kumzika marehemu katika Makaburi ya Mburahati jijini Dar, baba mzazi Alex Augustino alikaa kikao na ndugu ili kuangalia uwezekano wa kufika kwenye makazi hayo ya ubalozi na kuzungumza nao kujua hatima ya sakata hilo.

Baada ya makubaliano, familia hiyo ilielekea kwenye makazi hayo ambapo wengine walifikia nje kwanza,  Alex aliingia ndani kucheki usalama, yaani kama mbwa hao walikuwa eneo hilo au la! Kabla wengine hawajaingia.

“Kabla Alex hajamaliza kukagua, mbwa hao walimtoa mkuku. Ilikuwa na yeye ashambuliwe, ikabidi  aruke ukuta ili kutoka nje.

“Kitendo hicho kilimtia uchungu bibi wa marehemu, yaani mama wa Alex aliyekuwa kwenye gari ambapo alishindwa kuvumilia na kuangua kilio.

“Safari ya kuwaona wahusika wa ubalozi iliishia hapo. Wote walirudi nyumbani,” kilisema chanzo.

Chanzo chetu kiliendelea kudai kuwa baada ya kukaa kwa siku kadhaa, baba huyo wa marehemu alipigiwa simu na bosi wake akitakiwa kurudi kwani bado alitakiwa kuendelea kuishi mahali hapo akiwa msimamizi wa nyumba.

Habari zinadai kwamba, katika hali isiyokuwa ya kawaida, alipofika nyumbani hapo hakukuta mbwa hata mmoja.

Mpaka tunakwenda mitamboni balozi huyo hakupatikana lakini familia nayo inasisitiza kwamba wanataka kukutana na viongozi wa ubalozi na kujadili ni kitu gani kitaendelea.

0 Responses to “MBWA WALIOMLA MTOTO NA KUSABABISHA KIFO CHAKE NUSURA WAMLE BABA MTU.”

Post a Comment

More to Read