Tuesday, April 8, 2014

NAIBU WAZIRI MAENDELEO YA JAMII JINSIA NA WATOTO DKT PINDI CHANA AANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI NJOMBE.




Naibu waziri wa maendeleo ya jamii Jinsia na Watoto Pindi Chana leo ameanza ziara ya siku mbili mkoani Njombe kwa kutembelea vikundi vya Vikoba Makambako na vyuo vya maendeleo ya jamii Ulembwe na Njombe mjini ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wananchi kuwapeleka watoto wao kujiunga ili kupata elimu ya ufundi stadi ya kujitegemea Na kujipatia ajira kwa kujiajiri.

Akizungumza akiwa katika chuo cha maendeleo Ulembwe Naibu waziri Chana amewataka maafisa maendeleo kufanya kazi ya ziada kwa kutembelea na kutambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo vyuo vya ufundi stadi pamoja na kutoa elimu kwa jamii kutambua umuhimu wa kujiunga na vyuo hivyo.

Aidha Bi.Chana amepongeza kwa hatua za maendeleo zinazofanywa na wanachuo wa Ulembwe kwa kutoa fani  mbalimbali huku akichukua baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikivikabili  vyuo vya maendeleo ya Ufundi stadi hapa nchini na kwenda kuzifanyia kazi ambapo amesema pamoja na changamoto hizo vyuo hivyo vinatakiwa kubuni mbinu mbadala za kuweza kuwasaidia kupunguza baadhi ya changamoto zilizo chini ya uwezo wao.

Mkuu wa wilaya ya Njombe bi. Sarah Dumba pamoja na mambo mengine amemshukuru waziri wa wanawake,jinsia na watoto kwa kuwatembelea na kusikiliza kero zinazowakabili wanavyuo na vikundi vya akina mama na vituo vya watoto na kwamba huenda ikawa mwafaka kwa mkoa wa Njombe kupelekewa misaada na kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili.

Kwa upande wake katibu wa chama cha mapinduzi mkoa wa Njombe Hosea Mpagike amewapongeza vijana  na wazazi ambao wametambua  umuhimu wa kujiunga na vyuo hivyo ili kupatiwa elimu ya ufundi na kwamba hatua hiyo itasaidia kuwapatia uwezo wa kujitegemea   pindi watakapo kuwa uraiani  kwa manufaa yao.

Awali akisoma taarifa fupi kwa mgeni rasmi Mkuu wa chuo cha Maendeleo ya wananchi Ulembwe bwana Francis Haule amesema kuwa pamoja na serikali kuhamasisha vijana kujiunga na vyuo hivyo ili kujifunza ufundi stadi lakini bado wananchi wanamuamko mdogo wa kupeleka watoto wao katika chuo hicho ambapo mpaka sasa kina jumla ya wanachuo hamsini na tatu huku bado kinauhitaji mkubwa wa wanafunzi wa masomo ya ufundi.

Aidha bwana Haule amesema kuwa chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu ya umeme,upungufu wa watumishi,ukosefu wa usafiri,huku kikifanikiwa kutatua baadhi ya changamoto ikiwemo ujenzi wa maabara,kujenga mtambo wa gesi ya samadi kwaajili ya kupikia pamoja na kutoa fani mbalimbali za useremala, uashi, umeme wa nyumbani, ushonaji nguo, huku kikitoa masomo ya stadi za maisha, hisabati, kiingereza, uchoraji, ujasiliamali na kompyuta.

Kwa upande wao wanafunzi wa chuo hicho wameshukuru uongozi wa chuo cha Maendeleo cha wananchi Ulembwe kwa jitihada mbalimbali ambazo wamekuwa wakizifanya ili kukabiliana na changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza huku wakipongeza mkuu wa chuo kwani amekuwa msaada mkubwa kufanikisha maendeleo ya chuo hicho kwa kutafuta wafadhili mbalimbali kusaidia chuo hicho.

Ziara hiyo ya Naibu waziri Wanawake ,Jinsia na watoto  kesho inatarajia kuendelea katika Wilaya ya Ludewa  ambapo leo waziri huyo ametembelea kikundi cha wanawake UCLAS makambako ambacho kinashughulika na mikopo ya wananchi vijijini VIKOBA ambapo lengo la ziara hiyo ni kuwasikiliza wajasiliamali,vikundi na vyuo vya maendeleo na changamoto zake.

0 Responses to “NAIBU WAZIRI MAENDELEO YA JAMII JINSIA NA WATOTO DKT PINDI CHANA AANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI NJOMBE.”

Post a Comment

More to Read