Tuesday, April 8, 2014

WAANDISHI WA HABARI WAFUNDWA KUHUSU KATIBA MPYA.




WAANDISHI wa habari wametakiwa kuifahamu rasimu ya pili ya Katiba ili wasiipotoshe jamii wakati wa kupiga kura ya maoni.

Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya masuala ya usalama kwa waandishi wa habari.

Alisema katika mchakato huo kila kinachoandikwa kwenye vyombo vya habari wananchi wanaamini hivyo bila waandishi kuielewa vizuri rasimu jamii itapotoshwa.

“Jamani waandishi wenzangu tuisome vizuri rasimu hii na yale yanayopiganiwa katika Katiba… sisi ndio tutakuwa wa kwanza kulaumiwa pindi wananchi watakapokuja kufanya uamuzi mbaya.

“Kumbukeni Katiba ni maisha ya miaka 50 ijayo hivyo kwa kuwapotosha tutaipeleka nchi pabaya… ni muhimu tukasoma na kuelewa historia ya nchi hasa Muungano kabla ya kuandika na kutangaza kwenye vyombo vyetu,” alisema Kibanda.

Kwa mujibu wa Kibanda, wakati suala la muungano likiteka majadiliano ya katiba kwa sasa, suala hilo lilikuwepo siku nyingi hata waasisi wa muungano walilijua hilo.

Amesema kutoka na elimu ndogo iliyokuwepo awali, hata leo wanaopigania serikali tatu au mbili hawajui matatizo gani yapo kwenye muundo wanaoutaka, hawajui itawasaidia nini na kusisitiza kwamba waandishi ni bora warudi kwenye historia ya muungano ili kutoa elimu sahihi kwa jamii.

Kibanda alitumia fursa hiyo kumshauri rais atenge miaka mitano kwa ajili ya kueneza elimu ya Katiba kabla ya kuanza mchakato wa kupata Katiba mpya.

Kuhusu usalama wa waandishi wa habari, Kibanda alisema wanataaluma hao ni miongoni mwa makundi yanayosakawa huku akibainisha kwamba kauli tata zinazotolewa dhidi yao hasa na viongozi wa juu zinawafanya wanataaluma hao kudharaulika machoni mwa watu na kujengewa chuki katika jamii.

Miongoni mwa waandishi waliohudhuria semina hiyo ni Marine Hassan Marin, aliyesema suala la usalama kwa waandishi ni muhimu kutolewa mara kwa mara hata katika ofisi zao.

Kwa kipindi chote cha siku tatu walichokaa katika semina hiyo, Marin alisema amejifunza mambo mbalimbali kuhusu kujilinda wakati wa kutafuta habari ambayo awali alikuwa hayajui.

0 Responses to “WAANDISHI WA HABARI WAFUNDWA KUHUSU KATIBA MPYA.”

Post a Comment

More to Read