Monday, April 14, 2014
RAIS KIKWETE AMLILIA MAALIM GURUMO, ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI.
Do you like this story?
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella
Mukangara kufuatia kifo cha mwanamuziki maarufu na wa siku nyingi, Muhidini
Maalim Gurumo kilichotokea tarehe 14 Aprili, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliomsumbua
kwa muda mrefu.
“Nimesikitishwa na
kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Muhidini Maalim Gurumo ambaye alikuwa mmoja
wa wasanii wa muziki wa dansi nchini waliolitumikia Taifa hili kwa bidii tangu
miaka ya sitini kupitia sanaa ya muziki katika bendi mbalimbali za muziki wa
dansi kuanzia Bendi ya NUTA Jazz, Mlimani Park Orchestra, Orchestra Safari
Sound (OSS) na Msondo Ngoma ambayo ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013”, amesema Rais Kikwete
katika Salamu zake.
Rais Kikwete amesema mchango wa
Marehemu Muhidini Maalim Gurumo kwa Taifa letu ni mkubwa na wa kupigiwa mfano
kupitia kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu ambacho alikitumia kikamilifu
kwa manufaa ya wananchi wa nchi yetu na Taifa kwa ujumla.
Rais Kikwete amemuomba Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na
pole nyingi kwa familia ya Marehemu Muhidini Maalim Gurumo kwa kumpoteza
kiongozi na mhimili wa familia yao. Amesema binafsi anaungana na familia
ya marehemu kuomboleza msiba huu mkubwa kwa kutambua kuwa msiba wao ni wa wote,
na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema
peponi Roho ya Marehemu, Amina.
Aidha Rais Kikwete amewaomba wanafamilia
ya marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha
kuomboleza msiba wa mpendwa wao kwa kutambua kwamba yote ni mapenzi yake Mola.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
14 Aprili, 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS KIKWETE AMLILIA MAALIM GURUMO, ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI.”
Post a Comment