Thursday, June 12, 2014
MAHAKAMA YAELEZWA JINSI BILIONEA ERASTO MSUYA ALIVYOUAWA KINYAMA KWA KUTUMIA BUNDUKI YA SMG
Do you like this story?
Bunduki ya kivita aina ya Sub Machine
Gun (SMG) iliyotumika kumuua mfanyabiashara tajiri wa Mirerani, Erasto Msuya,
ilinunuliwa kwa Sh4 milioni nchini Kenya, Mahakama imeelezwa.
Imeelezwa pia kwamba wauaji wanne
waliokwenda eneo la tukio kutekeleza mauaji hayo, walilipwa Sh5 milioni kila
mmoja na washirika wao wakilipwa Sh3 milioni kila mmoja.
Hayo yamo katika maelezo ya mashahidi
57 kwa washtakiwa yalisomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa Kilimanjaro, Munga
Sabuni juzi na mawakili wa Serikali, Stella Majaliwa na Florentina Sumari
waliokuwa wakipokezana kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.
Msuya aliyekuwa anamiliki vitega uchumi
kadhaa, aliuawa kwa kumiminiwa risasi Agosti 7, mwaka jana saa 6:30 mchana
Mijohoroni wilayani Hai, Kilimanjaro na katika maelezo yake, mtaalamu
aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, Dk Paulo Christopher alisema ulikuwa
na matundu 26 ya risasi yaliyotokana na risasi 13 zilizoingia na kutokea upande
wa pili zikichanachana utumbo, mapafu, ubongo na bandama.
Ushahidi huo unadai kuwa katika eneo la
tukio, polisi waliokota maganda 22 ya risasi za SMG.
Mtaalamu wa makosa ya kijinai ya
kompyuta, Koplo William Obeid alieleza kuwa katika kufanikisha mauaji hayo,
laini mpya tano za Airtel zilisajiliwa kienyeji, zote zikiwa na jina la Motiti
Ndoole na laini iliyotumika kumvuta marehemu eneo la tukio ilikuwa 0682405323.
Katika ushahidi huo, Inspekta Samwel
Maimu alidai kuwa washtakiwa walikiri kosa na kueleza kuwa bunduki aina ya SMG
ilinunuliwa Namanga, upande wa Kenya. Inspekta Maimu alidai kuwa mshtakiwa wa
kwanza, Shariff Mohamed ndiye aliyetoa Sh4 milioni za kununua silaha hiyo na
kutoa fedha za kusajili line mpya tano za simu.
Pia alidai kuwa mshtakiwa huyo, ndiye
aliyetoa Sh3,350,000 zilizotumika kununulia pikipiki mbili moja aina ya Toyo na
nyingine King Lion zilizotumiwa na wauaji siku ya tukio.
Katika maelezo hayo yaliyosomwa
mahakamani, mshtakiwa wa kwanza (Shariff), anadaiwa kueleza namna alivyotoa
maagizo ya kusajiliwa kwa line mpya.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kueleza kuwa mshtakiwa
wa saba, Ally Mussa ndiye aliyemshauri atoe jiwe moja la Tanzanite
litakalotumika kumshawishi marehemu Msuya. Katika maelezo hayo, ilidaiwa kuwa
ndiye aliyelipa Sh4 milioni za kununua bunduki hiyo ya SMG na kwamba siku ya
tukio aliibeba kwa gari lake hadi eneo la tukio na kuwakabidhi wauaji.
Katika ushahidi huo, mshtakiwa wa tano,
Karim Kihundwa anadaiwa kueleza kuwa yeye ndiye aliyemmiminia risasi marehemu
ambazo hajui idadi yake na kwamba bunduki hiyo aina ya SMG waliinunua Namanga
na ilihifadhiwa nyumbani kwa Shariff sambamba na pikipiki zilizotumika.
Katika maelezo yake, mshtakiwa wa saba,
Ally Mussa au Majeshi anadaiwa kueleza kuwa ndiye aliyepewa kipande cha madini
na kwenda kumuuzia marehemu hotelini kwake SG Resort siku moja kabla ya mauaji.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kukikiri kuwa
siku hiyo alikwenda na vipande vitatu vya madini lakini akakataa kuuza vipande
viwili akisema yuko na wenzake na kukubaliana kufanya biashara siku inayofuata
na kwamba siku ya mauaji, yeye ndiye aliyemtumia ujumbe wa maandishi ya simu
marehemu na kukutana naye na kwenda naye hadi eneo la mauaji.
Katika maelezo yake shahidi huyo
anadaiwa kusema: “Tulipofika Mjohoroni, Erasto alishuka ili kukutana na Karimu,
mimi nikabaki kwenye gari, ndipo Karim akatoa bunduki na kuanza kummiminia
risasi Erasto.”
Alidai kuwa baada ya mauaji hayo,
alipakia pikipiki aina ya Toyo iliyokuwa ikiendeshwa na Karimu aliyekuwa na
bunduki hiyo ya SMG.
Mshtakiwa wa pili, Shaibu Jumanne
maarufu kama Mredii, anadaiwa kueleza kuwa Julai 26 mwaka jana, Shariff
alimfuata na kumweleza kuwa kuna kazi ya kumuua Erasto.
“Nilimweleza siwezi kuifanya ila
nitamtafutia vijana wa kufanya. Alinipa Sh300,000 na kunijazia mafuta ‘full
tank’ niende kuwatafuta Ally Majeshi na Jalila,” ushahidi huo umedai.
Kesi hiyo, imehamishiwa Mahakama Kuu ya
Tanzania na inasubiri kupangiwa Jaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MAHAKAMA YAELEZWA JINSI BILIONEA ERASTO MSUYA ALIVYOUAWA KINYAMA KWA KUTUMIA BUNDUKI YA SMG ”
Post a Comment