Thursday, June 12, 2014

SERIKALI YAWATOA HOFU WANANCHI KUHUSIANA NA NDEGE ZA MALAWI ZINAZOONEKANA MKOANI MBEYA




SERIKALI imesema kuwa ndege zinazoonekana mpakani mwa Tanzania na Malawi ni maalumu kwa ajili ya kufanya utafiti na vyombo vya udhibiti wa anga vimezipa vibali vya kuwa katika maeneo hayo.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Ileje, Aliko Kibona (CCM), aliyetaka ufafanuzi wa uwepo wa ndege hizo zinazoonekana zikizunguka katika wilaya za Ileje na Kyela.

Akitoa taarifa hiyo ya serikali, Waziri Mwakyembe alisema kuwa ndege hizo zipo kihalali, hivyo aliwataka wananchi wa maeneo hayo kutokuwa na wasiwasi.

“Serikali imejiridhisha kwamba hakuna ndege nyingine zaidi ya hizo za utafiti katika eneo hilo la nchi. Kilichokosekana hapa Msheshimiwa Spika ni taarifa sahihi ndani ya muda muafaka kwa wananchi, kuwa wategemee shughuli za kiutafiti za aina hiyo katika maeneo yao,” alisema Waziri Mwakyembe.

Alizitaja ndege hizo kuwa ni C-GSGJ Cessna 280, C-GSGL Cessna 280 na GSGL type 280 zinazofanya kazi ya kukusanya takwimu za kijiolojia nchini Malawi na zina vibali vyote vya TCAA kuruhusu ndege hizo zinazoruka chini chini kugeuzia ndani ya anga la Tanzania.
Ndege hizo ni mali ya Kampuni ya Sander Geophysics (T) Limited, yenye makao makuu yake Ottawa nchini Canada.

Aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi wanapoona matukio yasiyo ya kawaida katika maeneo yao.

0 Responses to “SERIKALI YAWATOA HOFU WANANCHI KUHUSIANA NA NDEGE ZA MALAWI ZINAZOONEKANA MKOANI MBEYA”

Post a Comment

More to Read