Thursday, June 12, 2014
BAJETI KUU YA SERIKALI KUSOMWA LEO BUNGENI DODOMA, WATANZANIA WAISUBIRIA KWA HAMU
Do you like this story?
Watanzania leo wanaelekeza macho na
masikio yao mjini Dodoma, kusikiliza Hotuba ya Bajeti ya Serikali,
inayotarajiwa kusomwa saa 10 kamili bungeni na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya
Salum.
Tayari Waziri Saada alishaeleza kuwa
makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2014/15, unaoanza Julai
mwaka huu, yatakuwa Sh trilioni 19.6 kutoka makadirio ya Sh trilioni 18.2 ya
Bajeti inayoisha muda wake.
Vipaumbele vya Bajeti hiyo, kwa maana
ya miradi itakayozingatiwa zaidi, ni iliyo katika Mpango wa Matokeo Makubwa
Sasa (BRN) unaohusisha sekta sita za Kilimo, Elimu, Maji, Utafutaji rasilimali
fedha, Nishati, Uchukuzi na Uboreshaji wa Mazingira ya kufanyia biashara na
Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano.
Akisoma mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo kwa mwaka 2014/2015, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na
Uratibu, Stephen Wassira, alisema mapendekezo ya mpango huo, yana vipaumbele
vitano.
Cha kwanza ni miundombinu, kikifuatiwa
na kilimo, viwanda vinavyotumia malighafi za ndani na kuongeza thamani,
maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi na uendelezaji wa shughuli za utalii,
biashara na fedha.
Katika hotuba hiyo, Watanzania wengi
watakuwa makini kusikiliza bidhaa na huduma zitakazoongezwa kodi, jambo
linalotarajiwa kuongeza bei ya bidhaa za huduma husika katika soko.
Katika bajeti inayoishia,
Serikali iliongeza kodi kwenye magari makuukuu, bia, vinywaji vikali na baridi
ambavyo kodi imekuwa ikiongezwa kila mwaka na kuwaathiri watumiaji.
Kutokana na hali hiyo wanywaji pombe na
sigara baada ya bajeti ya mwaka juzi ya 2012/2013, walilazimika kutumia fedha
nyingi ili kupata huduma hizo kwa kiwango kile kile katika mwaka huu wa bajeti
unaoisha.
Bidhaa zisizokuwa za mafuta ambazo
zilifanyiwa marekebisho na kuongezwa kodi ni mvinyo, pombe, vinywaji vikali, na
sigara.
Ushuru pia uliongezwa kwenye magari
yasiyokuwa ya uzalishaji na yenye umri wa miaka 10 kutoka asilimia 20 mpaka
asilimia 25.
Lengo la Serikali katika hilo, lilikuwa
kupunguza uagizaji wa magari chakavu ili kulinda mazingira na kupunguza ajali
za mara kwa mara.
Katika bajeti hiyo, vijana wa bodaboda
walicheka baada ya Serikali kusamehe ushuru wa barabara kwa pikipiki hizo za
biashara.
Moja ya kivutio kikubwa cha Bajeti
inayowasilishwa leo, ni matarajio ya wafanyakazi kuhusu utekelezaji wa ahadi ya
Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa katika sherehe za Mei Mosi mwaka huu, ya
kuongeza mshahara wa kima cha chini na kupunguza kodi ya mshahara (PAYE).
Rais Kikwete alisema Serikali
itaendelea kuongeza mshahara wa kima cha chini na kubainisha kuwa mwaka 2005
alipoingia madarakani, alikuta mshahara wa kima cha chini ni Sh 65,000 na
kukipandisha taratibu hadi kufikia Sh 240,000 cha sasa.
Kuhusu kupunguza PAYE, Rais Kikwete
alisema kusudi la Serikali ni kupunguza kodi hiyo ya mshahara kutoka asilimia
13 inayotozwa sasa, ifikie katika kiwango cha tarakimu moja.
Kuhusu misamaha ya kodi ambayo mwaka
huu imekuwa gumzo bungeni, huku wabunge wengi wakitaka ipunguzwe, Naibu Waziri
wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alinukuliwa akisema wafanyabiashara na vigogo
wanaokwepa kodi kwa kujificha kwenye mwavuli wa misahama, hawako salama.
“Tutafuatilia kikamilifu kwa kuwa wapo
watu wanaingiza bidhaa wanapewa msamaha, lakini ukija kwenye huduma za jamii
unakuta bidhaa hizo zinauzwa kibiashara,” alisema.
Mwigulu pia alizungumzia ukwepaji kodi
na matumizi mabaya ya fedha za Serikali na kufafanua kuwa, yatadhibitiwa.
“Bahati nzuri niliyonayo, sikuzaliwa na
chembe ya woga, kwa hiyo kwenye hili hakuna mkubwa wala mdogo, hakuna mtu
atagusa fedha ya umma kwa kukwepa au kwa kutumia vibaya kodi ambayo
ilishakusanywa halafu akapona asiguswe,” alisema.
Mwigulu alisema katika Bajeti ya
Serikali ya 2014/2015, yapo mambo ya msingi matano, ambayo yatasimamiwa
kikamilifu ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa tofauti na zilizopita.
Mbali na kuondoa misamaha ya kodi, pia
makusanyo ya ndani yatatiliwa mkazo zaidi ili kujenga uwezo wa kujitegemea
wenyewe badala ya kutegemea wahisani.
Jambo la tatu alisema ni kuhakikisha
Serikali inapeleka fedha kwenye mahitaji muhimu na kwa wakati, ili fedha za
maendeleo zitumike kama ilivyokusudiwa.
Jambo la nne litakalozingatiwa kwa
mujibu wa Mwigulu, ni usimamizi wa fedha zinazopatikana kwani pamoja na
makusanyo kidogo, lakini pia kuna uvujaji.
“Tunataka fedha inayopatikana na
kupangiwa kazi fulani itumike kwa shughuli iliyokusudiwa. Tutahakikisha
tunasimamia na kudhibiti matumizi yake,” alisema.
Naibu Waziri huyo wa Fedha alisema eneo
la tano ambalo litaangaliwa ni fedha ambazo hazitokani na kodi, bali
zinachangwa na wananchi na wadau wengine katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Alisema eneo hilo ni muhimu mbalo
Serikali inaona kuna haja ya kulisimamia vizuri, ili kuhakikisha fedha za
wananchi zinatumika vizuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BAJETI KUU YA SERIKALI KUSOMWA LEO BUNGENI DODOMA, WATANZANIA WAISUBIRIA KWA HAMU”
Post a Comment