Friday, June 13, 2014
KOCHA: KASEJA RUDI SIMBA, UNAMKUMBUKA MAXIMO?
Do you like this story?
BAADA ya Simba kumkosa kipa wa Yanga,
Ally Mustapha ‘Barthez’ ambaye amesaini mkataba mpya na timu yake, kocha wa
makipa wa Msimbazi, Iddi Pazi, amesema hakuna jinsi, haraka sana Juma Kaseja
anatakiwa kurudi Simba ili acheze kwa raha.
Kabla ya Yanga kumsainisha Barthez,
Simba ilikuwa imepiga hesabu za kumrudisha kipa wao huyo wa zamani ili apambane
na Ivo Mapunda ambaye hana mpinzani katika kikosi cha timu hiyo.
Kocha huyo alisema, kuna sababu tatu
zinazomfanya Kaseja kuondoka Yanga kwani akibaki hatoweza kufanya kazi yake kwa
furaha na mafanikio.
Alisema kwanza ushindani wa nafasi kati
yake na makipa Deo Munishi ‘Dida’ na Barthez ni mkubwa. Pili anaonekana
hakubaliki kwa mashabiki wa Yanga na tatu ni ujio wa kocha Marcio Maximo katika
kikosi hicho.
Pazi alisema: “Mahali alipo Kaseja
(Yanga), kunaweza kumfanya astaafu kabla ya muda wake au hata kuendelea kucheza
soka kwa mashaka hivyo namtaka afikirie kurudi Simba ili kutunza heshima na
kufanya kazi yake kama ilivyokuwa awali.
“Kaseja si kipenzi cha mashabiki Yanga
na inapokuja wakati wa kazi anaweza kupata wakati mgumu kutokana na kuzomewa na
kumfanya kutojiamini akiwa kwenye kazi yake.
“Pia nimesikia Yanga wanamleta Maximo,
nafikiri ni hofu kwa Kaseja kwa sababu siku za nyuma kocha huyo alitofautiana
naye wakiwa Taifa Stars, aje Simba ili awe na amani.”
Pazi pia amemtaka kipa huyo kufuta
ndoto za kustaafu soka wakati huu ili awe kocha akisema kipa huyo bado ana
uwezo wa kucheza.
“Nafikiri wapenzi wa Simba wanatakiwa
kumpa Kaseja nafasi kwenye mioyo yao. Amefanya mengi na naamini akirudi ataweza
kufanya mengi na kumalizia soka lake Simba akiwa na heshima,” alisisitiza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “KOCHA: KASEJA RUDI SIMBA, UNAMKUMBUKA MAXIMO?”
Post a Comment