Friday, June 13, 2014
PIKIPIKI ZOTE KUSAJILIWA UPYA, SASA KUPEWA NAMBA "TZ" BADALA YA "T"
Do you like this story?
Serikali imetangaza utaratibu mpya kwa
usajili wa namba za pikipiki kutoka ‘T’ na sasa zitasomeka ‘TZ’ lengo likiwa ni
kudhibiti vitendo vya uhalifu.
Hatua hiyo ilitangazwa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Uagizaji magari waongezwa makali
Waziri Mkuya alisema, Serikali
inatarajia kuongeza kodi kwa magari yatakayoingizwa nchini yakiwa yametumika
kwa zaidi ya miaka minane baada ya kubadilisha ukomo wa umri wa magari yasiyo
ya uzalishaji (non-utility vehicles) na magari ya uzalishaji na yasiyobeba
abiria (non-passenger utility vehicles), kutoka miaka 10 hadi minane.
Alisema hatua hiyo ina lengo la kulinda
mazingira na kupunguza wimbi la uigizaji wa magari chakavu ambayo yanasababisha
ajali, vifo na kuongeza gharama kwa kutumia fedha za kigeni kuagiza vipuri mara
kwa mara.
Pendekezo hilo pia liliwasilishwa
katika Bajeti inayomalizika lakini liliondolewa baada ya kuibua mvutano mkubwa
bungeni na kusababisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuingilia kati.
Waziri wa Fedha wakati huo, marehemu
William Mgimwa alisema Serikali iliwasilisha pendekezo hilo ili kupunguza muda wa
magari yaliyotumika kuingia nchini kwa lengo la kudhibiti magari chakavu,
kutunza mazingira na kuwapunguzia wananchi mzigo wa kununua mafuta kwa kuwa
yanatumia nishati hiyo kwa wingi.
Alisema Serikali inatekeleza hoja hiyo
kwa kuwa hata Kenya na Uganda wameanza kufanya hivyo na kwamba ni mpango wa
nchi nyingi.
Baada ya kuwasilisha muswada huo,
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, iliwasilisha maoni yake na
kupinga pendekezo hilo la Serikali kwa kueleza kwamba uwezo wa wananchi wengi
kununua magari mapya ni mdogo.
Akiwasilisha maoni ya Kamati, aliyekuwa
mwenyekiti wake, Andrew Chenge alisema Serikali haikuwa na nia ya kuyaondoa
barabarani magari yenye umri zaidi ya miaka 10, hivyo pendekezo hilo halikuwa
na manufaa kwa taifa.
“Kamati inaamini kwamba sababu
zilizofanya Serikali kuleta mapendekezo bungeni mwaka 2006 ya kutoza ushuru wa
bidhaa za magari yenye umri zaidi ya miaka 10 bado zina nguvu hadi leo… Kamati
inashauri umri wa magari yanayostahili msamaha uwe miaka 10 na siyo minane inayopendekezwa,”
alisema.
Msimamo huo wa Kamati uliungwa mkono na
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambayo ilisema hoja ya Serikali katika eneo
hilo ni dhaifu kwa kuwa wananchi wengi hata wabunge hawana uwezo wa kununua
magari mapya na wala umri wa gari si kigezo pekee cha ubora.
Mvutano huo ulimlazimu Waziri Mkuu
Pinda kuingilia kati na kueleza kwamba Serikali imekubaliana na maoni ya
wabunge na kukubali umri wa magari yanayoingia nchini kubaki kuwa miaka 10.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “PIKIPIKI ZOTE KUSAJILIWA UPYA, SASA KUPEWA NAMBA "TZ" BADALA YA "T" ”
Post a Comment