Saturday, June 14, 2014

MADUDU KWENYE BAJETI 2014/2015



Serikali imeendeleza usiri kuhusu gharama halisi za uendeshaji wa Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na gharama hizo kutowekwa wazi katika vitabu vyote vya makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/15.

Bunge Maalumu la Katiba linatarajiwa kukutana kwa mara ya pili kuanzia Agosti, baada ya kuahirishwa  Aprili ili kupisha vikao vya Bunge la Bajeti ambavyo vinaendelea mjini Dodoma hivi sasa.
Uchambuzi uliofanywa katika vitabu vya bajeti unaonyesha kuwa fedha za kugharimia Bunge la Katiba zimetengwa chini ya fungu namba 21 ambalo ni Hazina katika kipengele ambacho kinajumuisha utekelezaji wa masuala mengine kadhaa.

Kitabu namba mbili ambacho kimechambua makadirio ya matumizi ya Serikali kinaonyesha kuwa zaidi ya Sh227.725 bilioni, zimetengwa chini ya kifungu namba 290700 kinachoitwa Contingency Non-Emergency (mambo yanayoweza kutokea ambayo siyo dharura), huku ufafanuzi kwenye randama za Hazina zikionyesha Bunge la Katiba ni moja ya mambo hayo.

“Matumizi katika eneo hili yanajumuisha gharama za upigaji kura za maoni ili kupitisha Katiba Mpya, kuboresha Daftari la Wapigakura kwa ajili ya uchaguzi ujao, kulipa madeni ya makandarasi na watumishi na gharama za kuendesha Bunge la Katiba,” inasomeka sehemu ya randama ambayo iliwasilishwa bungeni ikifafanua matumizi ya fedha zilizoombwa na kuendelea:
“Makubaliano mapya ya PAYE kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nyongeza ya gharama za shule, mitihani, bweni  na ukaguzi wa shule za msingi na sekondari, mchango wa Serikali kwenye capitation: gharama za ujenzi katika maeneo mapya ya utawala, stahili za waajiriwa wapya katika mamlaka za serikali za mitaa.”

Maeneo mengine yanayotajwa katika randama hiyo ni deni la michango ya watumishi wa PSPF, mfuko wa jimbo, michango katika taasisi na mashirika ya kimataifa, deni la HESLB kwa mfuko wa PSPF, deni la Ukumbi wa Bunge kwenye Mfuko wa NSSF, on call allowance (posho) kwa ajili ya hospitali za mikoa na wilaya, pamoja na madeni ya mashirika.

Hata hivyo wakati kukiwa na maelezo hayo, randama za makadirio ya matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonyesha kuwa Idara ya Ukaguzi wa Shule ambayo inahusika na ukaguzi wa shule za msingi na sekondari imetengewa kiasi cha Sh9,542,456,924 katika mwaka ujao wa fedha.

Kati ya hizo Sh8,792,456,924 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh750,000,000 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo itakayojumisha ukaguzi wa shule na ukarabati wa ofisi za ukaguzi wa shule katika Kanda za Ziwa na Nyanda za Juu Kusini na Halmashauri za Wilaya za Bagamoyo, Sumbawanga, Hai, Urambo na Chunya.
Via<Mwananchi.

0 Responses to “MADUDU KWENYE BAJETI 2014/2015”

Post a Comment

More to Read