Saturday, June 14, 2014
YULE KIGOGO WA TANESCO AMKANA MKEWE MAHAKAMANI.
Do you like this story?
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi William Mhando, ameieleza Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuwa mshitakiwa wa pili (Eva Mhando) katika kesi
ya matumizi mabaya ya madaraka, si mke wake.
Mhandisi Mhando alitoa madai hayo jana
mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi, alipokuwa akisomewa maelezo ya awali katika
kesi hiyo na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru),
Leonard Swai.
Mhando alikiri maelezo kuwa alikuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco tangu Juni 2010 hadi 2012, lakini alikana maelezo
kuwa mshitakiwa wa pili (Eva Stephen Mhando) ni mkewe ambaye pia ni Mkurugenzi
Mkuu wa Kampuni ya Santa Clara Supply Limited.
Kwa upande wake, Eva alikubali
kwamba aliwahi kuajiriwa na Tanesco kuanzia mwaka 1982 hadi 2009, mshitakiwa wa
tatu, France Mchalenge pia alikubali kwamba alikuwa mwajiriwa wa shirika hilo,
wakati uchunguzi unafanyika alikuwa mhasibu mkuu na alikuwa mjumbe wa Kamati ya
Tathimini ya Zabuni namba Pa/001/11/HQ/G/011 ya vifaa vya ofisi, ikiwemo printa
na kompyuta.
Swai alidai mshitakiwa wa nne, Sophia
Misidai aliajiriwa na Tanesco na wakati uchunguzi unafanyika alikuwa mhasibu
mkuu na mjumbe wa kamati iliyofanya tathimini ya zabuni ya kusambaza vifaa vya
ofisi katika shirika hilo. Mshitakiwa alikubaliana na maelezo hayo.
Mshitakiwa wa tano, alikubali kwamba
alikuwa mwajiriwa wa Tanesco na kuwa wakati wa uchunguzi alikuwa ofisa
usambazaji na alikuwa mjumbe wa kamati iliyotathimini zabuni hiyo.
“Mheshimiwa Hakimu, Kampuni ya Santa
Clara Supply Ltd inamilikiwa na Eva Stephen William, Fred William na Veronica
Stephen Mhando, ilipata zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi yenye thamani ya sh
milioni 884.5.
“Mhando akiwa Mkurugenzi Mkuu wa
shirika hilo na Eva akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Santa Clara Supply Ltd alisaini
barua ya kuipa zabuni huku akijua wazi kwamba kampuni hiyo inamilikiwa na
familia yake, pia hakujitoa kuonyesha kwamba ana maslahi na kampuni hiyo,”
alidai.
Wakili Swai aliendelea kueleza kuwa
Mhando aliwapa zabuni hiyo mshitakwa wa pili, Eva na watoto wake kinyume na
utaratibu, walitaka kuiuza kampuni hiyo kwa mtu mwingine wakati tayari
walishapata zabuni ya kusambaza vifaa hivyo vya ofisi, mshitakiwa wa kwanza
(Mhando) alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kuonyesha kwamba ana
maslahi binafsi na Kampuni ya Santa Clara,” alidai Swai.
Swai alidai kwamba Eva alighushi
taarifa za ukaguzi wa hesabu za Kampuni ya Santa Clara ya mwaka 2007/2008
akionyesha kuwa Kampuni ya Finx Capital House ilifanya ukaguzi.
Pia mshitakiwa huyo alighushi taarifa
ya kuhamisha hisa akionyesha hisa 200 zenye thamani ya sh 10,000 zilihamishiwa
kwa Eveta Shing’oma.
Eva alidaiwa kutoa taarifa ya ukaguzi
wa fedha kwa Katibu wa Bodi ya Zabuni wa Tanesco akionyesha zilifanyiwa ukaguzi
Desemba, mwaka 2010, akajipatia sh milioni 37.7 kutoka kwa shirika hilo.
Swai alidai Mchalange, Misidai na
Naftali Kisinga walitoa taarifa katika Bodi ya Zabuni kuonyesha kwamba Kampuni
ya Santa Clara walikuwa wana sifa ya kupata zabuni hiyo, walipata mkataba wa
kusambaza vifaa vya ofisini wenye thamani ya sh 884,550,000. Washitakiwa hao
walikana maeneo yote hayo.
Wakili Swai alieleza upande wa jamhuri
unatarajia kuleta mashahidi 14 na wanawasilisha mahakamani vielelezo 18.
Hakimu Mushi aliahirisha kesi hiyo hadi
Julai 29-30, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
>>TANZANIA
DAIMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “YULE KIGOGO WA TANESCO AMKANA MKEWE MAHAKAMANI.”
Post a Comment