Monday, July 21, 2014

WALIOUA KWA DENI LA SHILINGI 9,600 WANYONGWA WILAYANI ROMBO.




WATU watatu wakazi wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wamehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mauaji.

Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Moshi iliyokuwa ikiendesha vikao vyake katika Mahakama ya Wilaya ya Rombo chini ya Jaji Amaisario Munisi.

Awali kabla ya kusoma hukumu hiyo, Mwanasheria wa Serikali, Tamari Mndeme aliwataja watuhumiwa hoa kuwa ni Plasid Herman, Wiliadi Evaristi na Samsoni Kanje Myovela wanaokabiliwa na tuhuma za kumuua kwa makusudi mkazi wa Kijiji cha Nayeme Tarafa ya Tarakea, Anastazia Nicodemu.

Alisema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Mei 23, 2010 katika Kijiji cha Nayeme Tarafa ya Tarakea wilayani Rombo, ambapo imedai kuwa watuhumiwa hao walimuua kwa makusudi, Bi. Nicodemu kinyume na kifungu cha 196 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akisoma hukumu yao, Jaji Munisi ambaye alianza majira ya saa 14:21 mchana na kukamilisha saa 15:26 ameisema katika kesi hiyo upande wa mashtaka na utetezi haubishaniwi kuhusu kifo cha marehemu.

Alisema katika kutetea hoja zao upande wa mashtaka ulileta mashahidi 6 ambao wote kwa pamoja wakiongozwa na shahidi namba moja waliwatuhumu washtakiwa kuhusika na tukio hilo.

Alinukuu kielelezo namba Moja kilichowasilishwa na hakimu mkazi wa mahakama ya mwanzo Usseri ambaye alimwandikia maelezo ya ungamo ambapo Mshtakiwa namba tatu alikiri kuwa yeye na wenzake wawili walienda nyumbani kwa marehemu majira ya saa tatu usiku kwa ajili ya kwenda kumdai fedha yao kiasi cha tsh 9600 ikiwa ni malipo yao ya kupukuchua mahindi lakini walipofika walimkosa nyumbani na hivyo wakapanda ukuta wa nyumba na kuingia ndani ambapo walijificha uvunguni mwa kitanda chake na aliporudi walimshambulia kwa mapanga na kusabababisha kifo chake.

Kutokana na ushahidi huo alisema Mshtakiwa namba moja na namba mbili wanatiwa hatiani kuhusika moja kwa moja na mauaji kutokana na ukiri wao kwa mlinzi wa amani, Mchukua maelezo na shahidi namba tatu ambaye ni mume wa marehemu ambaye anadai kuwa alishuhudia wakitekeleza tukio hilo na kuwatambua wahusika Kutokana na utetezi huo, Jaji Munisi alisema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kuthibitisha kuhusika pasipo shaka kwa washtakiwa wote watatu kwa mujibu wa sheria kifungu cha 197 ya sheria ya kanuni ya adhabu washtakiwa hao adhabu yao ni kunyongwa hadi kufa.

0 Responses to “WALIOUA KWA DENI LA SHILINGI 9,600 WANYONGWA WILAYANI ROMBO.”

Post a Comment

More to Read