Monday, September 8, 2014
TUME YA OPARESHENI TOKOMEZA UGAIDI YAANZA KAZI KUBAINI MATESO WALIYOTENDEWA WANANCHI.
Do you like this story?
Tume iliyoundwa na
Rais Jakaya Kikwete kuchunguza vitendo vilivyotokana na utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza Ujangili nchini, imeanza rasmi kazi kwa kupokea taarifa na
malalamiko mbalimbali kuhusu operesheni hiyo.
Aidha, katika
kufanikisha majukumu yake, Tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji na
Balozi mstaafu Hamisi Msumi, itatembelea maeneo mbalimbali nchini ili kukutana
na wananchi wenye taarifa au malalamiko kuhusiana na jinsi Operesheni Tokomeza
ilivyofanyika.
Hayo yameelezwa na
Katibu wa Tume hiyo, Frederick Manyanda katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari, jana.
Taarifa hiyo imeeleza
kuwa, taarifa au malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa operesheni hiyo
yatapokelewa kwa njia mbalimbali, zikiwemo kwa posta, baruapepe na hata simu za
mkononi.
Amezitaja namba
zitakazotumika kuwa ni 0714 826 826, 0767 826 826, 0787 826 8265 na 0773 826
826. Aidha, baruapepe ni opereshenitokomeza@agctz.go.tz na kwa watakaopenda
kutoa taarifa au malalamiko kwa njia ya barua, watalazimika kupitishia barua
zao kwa Katibu wa Tume, Tume ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili,
S.L.P 9050, Dar es Salaam.
Tume hiyo iliundwa na
kutangazwa Mei 2 mwaka huu na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue
kuwa, Rais ameunda Tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha Sheria ya
Uchunguzi Sura ya 32.
Hatua ya Rais Kikwete
kuunda tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha Sheria ya Uchunguzi, Sura
ya 32 ilikuja baada ya Operesheni Tokomeza Ujangili kusitishwa na Bunge kutokana
ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu wakati wa utekelezaji wake.
Operesheni hiyo
iliyoanza Oktoba mwaka 2013 na kusitishwa Novemba 4 mwaka jana, ndiyo
iliyowang’oa mawaziri wanne kwa kile kilichodaiwa kushindwa kusimamia vizuri
utekelezaji wake.
Mawaziri hao ni
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maliasili na Utalii,
Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo
David Mathayo.
Wakati wa kutangaza
tume hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliyataja majukumu ya tume
hiyo kuwa ni pamoja na kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza
ilivyoendeshwa.
Majukumu mengine ni
kuchunguza na kubaini iwapo Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu za Rejea
zilifuatwa na watu waliotekeleza Operesheni Tokomeza na kuchunguza na kubaini
iwapo yupo mtu yeyote aliyekiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea wakati wa
Operesheni Tokomeza.
Kuchunguza na kubaini
kama wapo watu wowote waliokiuka Sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza na kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao
zilikuwa stahiki.
Kupendekeza hatua
zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kukiuka Sheria,
Taratibu na Hadidu za Rejea za Operesheni Tokomeza.
Kupendekeza mambo ya
kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili
kuepuka kasoro.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TUME YA OPARESHENI TOKOMEZA UGAIDI YAANZA KAZI KUBAINI MATESO WALIYOTENDEWA WANANCHI.”
Post a Comment