Friday, November 14, 2014

HATURUHUSU WAFUNGWA KUFANYA TENDO LA NDOA GEREZANI,WIZARA YA MABO YA NDANI.





SERIKALI imesema Tanzania haina sheria ya kuwaruhusu wafungwa kukutana faragha na wenzao wao.

Hii ni mara ya tatu kwa serikali kutoa majibu hayo, kutokana na maswali ya wabunge ambapo mara kadhaa swali hilo limekuwa likiulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Salum Msabaha (Chadema).

Hata hivyo, jana Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alikiri kwa Tanzania kutokuwa na sheria hiyo na akajibu kuwa ujauzito ambao huwapata wafungwa wanawake, unatokana na wafungwa hao kuupata nje ya Magereza.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Maalumu, Rukia Kassim Ahmed (CUF) ambaye alitaka kujua ni kwa namna gani wafungwa wanawake wanapata ujauzito wanapokuwa ndani ya magereza yao.

Pia, alihoji kama magerezani kuna usiri, ni kwa namna gani mahabusi ambao ni mashekhe kutoka Zanzibar wanafanyiwa vitendo vya ulawiti gerezani.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema jeshi la Magereza lina utaratibu wa kutenganisha wafungwa wa kiume na wa kike kwani kila watu hutunzwa kwa sehemu zao na hulindwa na watu wa jinsia zao.

Kuhusu tuhuma za kulawitiwa kwa mashekhe wa Zanzibar, Waziri wa Mambo ya Ndani Mathias Chikawe, alisema sakata la Shekhe Salum Ali Salum linafanyiwa kazi na kwamba kiongozi huyo ameshafanyiwa uchunguzi wa awali katika Hospitali ya Amana.

“Jambo hilo lipo mikononi mwetu, tumempeleka Hospitali ya Amana na kesho (leo) tutampeleka Hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi, lakini tunachunguza pia tabia ya kiongozi huyo na mwenendo wake kabla ya kuingia gerezani,” alisema Chikawe.

Hata hivyo, Chikawe alisema kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwa watuhumiwa hao, kwani tangu mwanzo hakuwa ameripoti vitendo hivyo, lakini alipofika mara ya nne gerezani ndipo akaripoti kufanyiwa vitendo hivyo na mmoja wa polisi.

0 Responses to “HATURUHUSU WAFUNGWA KUFANYA TENDO LA NDOA GEREZANI,WIZARA YA MABO YA NDANI.”

Post a Comment

More to Read