Thursday, November 13, 2014

KONDOMU ZAZUA KIZAAZA NCHINI TANZANIA.




 Imeelezwa kuwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), yanaweza kuongezeka nchini hasa kwa vijana kutokana na kubainika kupungua kwa kasi ya matumizi ya mipira (kondomu).

Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens Turuka katika mkutano wa sita wa kutathmini maambukizi ya VVU nchini.
 
Dk Turuka amesema maambukizi mapya yameendelea kuwapo kwa sababu vijana hawatumii kondomu kujikinga.
“Matumizi ya kondomu katika jamii yamepungua na kuwafanya watu wengi hasa vijana kupata maambukizi na zaidi ni kutokana na mwamko mdogo kuhusu umuhimu wa kondomu kama kinga ya Ukimwi,” amesema.

Alisema utafiti uliofanyika mwaka jana ulionyesha kuwa asilimia 50 ya waliojitokeza kupima VVU na kupata ushauri, walikiri kutotumia kondomu. Hata hivyo, Dk Turuka alisema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, maambukizi mapya yalipungua kutoka watu 180,000 hadi 72,000 kwa mwaka.

Amesema licha ya kuwapo mafanikio hayo, kiwango cha matumizi ya kondomu kimeshuka na kuhatarisha maisha ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 – 39.

Amesema mwaka ujao wa fedha, Serikali itaanzisha mfuko maalumu wa kukusanya fedha kwa ajili ya kununulia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARV).

Amesema zaidi ya nusu ya wagonjwa walioathirika wanahitaji dawa hizo.

Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Fatma Mrisho alisema wanafanya jitihada kuhakikisha wanapunguza maambukizi mapya hadi kufikia sifuri ifikapo mwaka 2020.


Aliitaja baadhi ya mikoa yenye idadi kubwa ya maambukizi mapya kuwa ni Njombe, Shinyanga, Mbeya, Dar es Salaam na Ruvuma.
“Katika miaka miwili ijayo, tutaelekeza nguvu zetu kwenye mambo yanayochangia kuongezeka kwa maambukizi mapya, ikiwamo maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kukabiliana na uhaba wa dawa,” amesema.

Na Peter Elias, Mwananchi

0 Responses to “KONDOMU ZAZUA KIZAAZA NCHINI TANZANIA.”

Post a Comment

More to Read