Thursday, November 20, 2014
TAMISEMI YATANGAZA TAREHE YA KUJIANDIKISHA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
Do you like this story?
Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa Bwana Kharist Michael Luanda amesema wananchi wanapaswa kujiandikisha katika daftari maalum la kupigia kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanzia tarehe 23/11/2014 hadi tarehe 29/11/2014.
Mkurugenzi
huyo alisema kuwa wananchi wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi
katika ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa wanapaswa kuchukua fomu za kugombea
kuanzia tarehe 16/11/2014 hadi tarehe 22/11/2014. Akizungumza na waandishi wa
habari mjini Dodoma, Bwana Luanda aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi
katika zoezi la kujiandikisha ili waweze kupata fursa ya kushiriki katika
kupiga kura ili kuwachagua viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa wanaowataka.
Alisema sifa
za mtu anayestahili kujiandikisha kushiriki uchaguzi huo ni lazima awe raia wa
Tanzania, mwenye umri wa miaka 18 au zaidi, mkazi wa eneo hilo na mwenye akili
timamu.
Pia
alisisitiza kuwa uandikishaji huo utafanyika katika vituo maalum
vilivyoandaliwa ambavyo vipo katika majengo ya umma, isipokuwa sehemu ambazo
hazina majengo hayo, uandikishaji utafanyika katika vituo maalum kutokana na
makubaliano ya Msaidizi wa Uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa.Bwana Luanda
amesisitiza kuwa vituo hivyo vitafunguliwa saa 1:30 asubuhi na kufungwa saa
10:30 jioni.
Aidha
alisema kuwa vyama vya Siasa vitaruhusiwa kuweka mawakala wao wakati wa
uandikishaji wa wa wapiga kura lakini gharama za kuwalipa zitakuwa
juu ya chama husika. Kuhusu sifa za mtu anayetaka kugombea nafasi
mbalimbali katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mtaa Mkurugenzi huyo alisema
kuwa ni lazima awe mtanzania mwenye umri wa miaka 21 au zaidi na awe mkazi wa kudumu wa eneo
husika.
Vile vile
alisema kuwa wasimamizi wasaidizi wa kila kituo wanapaswa kubandika
orodha ya wapiga kura tarehe 30/11/2014, endapo mkazi yeyote au chama cha siasa
kitakuwa na pingamizi au maoni juu ya orodha hiyo basi awasiliane na msimamizi
msaidizi wa uchaguzi ili kuweza kufanyia marekebisho na orodha ya mwisho
itabandikwa siku tatu kabla ya uchaguzi.
Uchaguzi wa
serikali za Mitaa Tanzania Bara umepangwa kufanyika disemba 14, 2014, ambapo
wananchi watawachagua wenyeviti wa vijiji, vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa
Halmashauri za vijiji na Wajumbe wa Kamati za Mitaa.
Viongozi
watakaochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni pamoja na wajumbe wa
Halmashauri ya Kijiji wasiopungua 15 na wasiozidi 25, wenyeviti wa Mitaa na
wajumbe wa kamati za Mitaa wasioziidi 6 na wenyeviti wa vitongoji wa kila
kitongoji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TAMISEMI YATANGAZA TAREHE YA KUJIANDIKISHA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA ”
Post a Comment