Wednesday, January 7, 2015

AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA JELA KWA KOSA LA KUMLAWITI MTOTO WA MIAKA 5




Na Joachim Nyambo,Mbarali.

MAHAKAMA ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imemhukumu kifungo cha maisha jela mkazi wa Madibira wilayani hapa kwa kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka mitano.

Aliyehukumiwa kutumikia kifungo hicho ni Samwel Mnyonge(30) ambapo hukumu hiyo imetolewa na hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Mbarali Guwai Sumaye.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa jeshi la polisi Mazoya Luchagula mbele ya hakimu mfawidhi Sumaye kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Februari 11,2014 kijijini Madibira wilayani hapa.

Mazoya alisema awali mshitakiwa alimbeba mtoto huyo wa umri wa miaka mitano kwenye baiskeli akiwa amempa msaada wa kumrejesha nyumbali alipokuwa akitokea shuleni lakini wakiwa njiani,Mnyonge alimpeleka mtoto kwenye shamba la mahindi na kumlawiti.

Alisema kutokana na majeraha makubwa aliyoyapa mtoto huyo,ilibidi ndugu na jamaa kumkimbiza katika hospitali ya Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa na baadaye mtoto huyo kupelekwa hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam alikokaa kwa muda wa miezi nane kwaaajili ya matibabu.

Akitoa hukumu baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo,hakimu mfawidhi Guwai Sumaye amesema anamhukumu Mnyonge kwenda jela kutumikia kifungo cha maisha ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia hiyo.

Mwisho.

0 Responses to “AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA JELA KWA KOSA LA KUMLAWITI MTOTO WA MIAKA 5”

Post a Comment

More to Read