Tuesday, January 6, 2015
UAPISHAJI WENYEVITI WA MITAA NA WAJUMBE ULIVYOINGIA DOSARI JIJINI MBEYA.
Do you like this story?
Kaimu mwanasheria wa halmashauri ya jiji la Mbeya Chrispin Kaijage akigawa fomu za kiapo kama njugu nje ya ukumbi hali iliyosababisha hata wasiopaswa kuapishwa kuchukua fomu hizo. |
Haikujulikana mara moja maboksi haya yalikuwa na nini ndani.Yaliondolewa ukumbini mara baada ya wajumbe kukasirika na kuamua kutoka nje ya ukumbi. |
Wajumbe wakiwa wametawanyika mara baada ya kutoka nje ya ukumbi(picha na joachim Nyambo>Lyamba lya Mfipa) |
KATIKA kile kinachodhihirisha uwepo wa baadhi ya watendaji
ambao wamekuwa wakisababisha serikali kuchukiwa na wananchi kwa kuvurunda
kwenye maeneo yao,kaimu mwanasheria wa halmashauri ya jiji la Mbeya Chrispin
Kaijage jana(Januari 5) alivuruga shughuli ya kuwaapisha wenyeviti na wajumbe
wa serikali za mitaa.
Shughuli hiyo iliyokuwa ianze majira ya saa tano asubuhi
katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Mbeya Day jijini hapa,shughuli hiyo
ilionekana kuanza kuingia dosari tangu mapema na hali hiyo kuendelea hadi
tunakwenda mitamboni.
Dosari ya kwanza ilianza pale Kaijage aliporuhusu shughuli
hiyo kugeuzwa na kuwa mkutano wa kisiasa ukiongoza na mmoja wa viongozi wa
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa) Baraka Mwakyabula ambaye
ni katibu mwenezi wa Chadema Mbeya mjini.
Chini ya mwanasheria huyo,Mwakyabula alikabidhiwa ukumbi na
kuendesha mkutano atakavyo kwani ndiye aliyeweza kuchagua wajumbe aliotaka
wasimame na kuuliza maswali yaliyoikuwa yakijibiwa na mwanasheria wakati
wajumbe wakisubiri viongozi wa halmashauri wafike kuwaapisha.
Ni wakati huop ambapo baadhi ya wajumbe walionekana kukerwa
na kile kilichoendelea ukumbini hapo kiasi cha kumtaka mwanasheria aharakishe
kuwaleta viongozi wa halmashauri ili waapishwe na kuondoka ili wakaendelee na
shughuli zao nyingine.
Wajumbe walionekana kusononeshwa zaidi kwa mwanasheria
kuendelea kuruhusu shughuli ya kuapishwa ambayo ilikuwa ikiendelea kuchelewa na
kugeuzwa kuwa mkutano wa kisiasa kwani hata katika kuteua wajumbe wa kuuliza
mwongozaji alikuwa akionekana kutoa nafasi zaidi kwa wajumbe kutoka vyama vya
upinzani na kuwanyima fursa wanaotoka CCM.
Siasa hizo zilizokwenda sambamba na kuchelewa kwa mkurugenzi
wa halmashauri ya jiji Musa Zungiza kulizidi kuingiza dosari shughuli nzima
kwani ilipofika majira ya saa nane kasoro wajumbe walichukua uamuzi wa kuanza
kutoka nje ya ukumbi na hapo kila mmoja akawa anaongea kwa jazba maneno
aliyoona yanafaa.
Wakizungumza kwa jazba nje ya ukumbi wajumbe hao walisema
Mkurugenzi wa Jiji na uongozi wa Halmashauri kwa ujumla umewadharau na
kuwanyanyasa kutokana na kutofuata muda waliokuwa wamewaandikia awali.
Mwakyabula ambaye pia ni mwenyekiti wa Mtaa wa Mwanjelwa
alimgeuka mwanasheria na kuungana na wajumbe wenzake kulalamika akisema katika
barua ya Halmashauri ya Jiji ya kuwaita kuapishwa ilidai wanapaswa kufika eneo
la tukio kuanzia majira ya saa tano asubuhi jambo ambalo lilitekelezwa kwa
wakati lakini wahusika hawakufika katika muda ulioandikwa.
“Kitendo hiki ni kuonesha dharau kwa wenyeviti na
wajumbe.Haiwezekani wakatuita saa tano asubuhi lakini hadi hivi sasa ni saa
nane mchana hawajafika, hii ni fedheha kubwa hivyo tumekubaliana zoezi hili
liahirishwe kwa leo hadi siku nyingine watakapojipanga” alisisitiza Mwenyekiti
huyo.
Hata hivyo alisema licha ya kuahirisha kwa shughuli hiyo ya
kuapishwa lakini uongozi wa halmashauri ya Jiji la Mbeya unapaswa kuwaomba
msamaha wajumbe kwa kuwadharirisha pamoja na kuwalipa posho ya siku hata kama
zoezi halikufanyika.
Wakati hayo yote yakiendelea wajumbe walikuwa wamegawanyika
ambapo kundi kubwa walikuwa nje na wachache walisalia ndani ya ukumbi
wakiendelea kusubiri na hapo ndipo ilikuja dhana ya kuwa waliobakia ukumbini ni
wanaccm na baadhi ya wajumbe waliokuwa nje wakaanza kusuka mpngo wa kuingia
wawapige ili kuwalazimisha kutoka nje.
Wakati hayo yakiendelea,punde kaimu mwanasheria alionekana
akiwa katika lango kuu(Getini) na akaanza kugawa fomu kiholela kwa wajumbe
waliokuwa jirani hali iliyosababisha wajumbe wote waliokuwa nje kukimbilia eneo
la getini na kuanza kugawana fomu za kiapo kama njugu.
Wapo wajumbe walioonekana kuchukua fomu zaidi ya kumi na
kuanza kuwagawia wenzao lakini wapo pia ambao walichukua fomu kwa kiasi hicho
na wakaonekana kutoka nje ya geti na kuelekea makwao pasipo kueleza fomu hizo
walikuwa wakizipeleka wapi.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wajumbe kuhoji ni kwa namna
gani udhibiti wa fomu hizo umewekwa kwakuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa
fomu kujazwa na mtu asiyestahili.
Kwa upande wake Kaijage, ambaye alikuwa akiwasihi wajumbe
kutulia lakini alishindwa kutoa ufafanuzi juu ya sababu ya kuchelewa kwa
viongozi waliopaswa kuwaapishwa Wenyeviti hao pamoja na wajumbe wao.
Aidha alipoulizwa na waandishi wa habari sababu za yeye
kuanza kugawa fomu za kiapo kiholela pasipo kufuata utaratibu huku akianzia
barabarani alijibu kuwa yeye sie msemaji bali alifika kituoni hapo kushuhudia
zoezi la kuwaapisha viongozi hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya,
Musa Zungiza, alipofuatwa ofisini kwake,wanahabari walijibiwa kuwa alikuwa nje
ya ofisi katika shughuli za kuapisha wajumbe na wenyeviti kwenye kanda nyingine
na alipotafutwa kwenye simu yake ya kiganjani kujibu changamoto iliyojitokeza
hakuweza kupokea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “UAPISHAJI WENYEVITI WA MITAA NA WAJUMBE ULIVYOINGIA DOSARI JIJINI MBEYA.”
Post a Comment