Thursday, March 5, 2015
MAPACHA WA MAKETE WALIOUNGANA KUINGIA KIDATO CHA TANO.
Do you like this story?
Mapacha walioungana kiwiliwili,
Consolata na Maria Mwakikuti (18), wa Kijiji cha Ikonda wilayani Makete mkoani
Njombe, wamefaulu mtihani wao wa kuhitimu kidato cha nne kwa alama sawa
isipokuwa masomo mawili.
Ufaulu wao wa alama ya Credit 2.0, huku
wakiwa wamefanya vizuri katika Kiingereza na Bayolojia, umekuja wakati
wanafunzi wengi wa shule ya Sekondari Maria Consolata iliyoko
mkoani Njombe, wakiwa wamefanya vibaya katika matokeo ya mwaka jana.
Kutokana na alama walizopata,
zinawawezesha Maria na Consolata kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano, Julai
mwaka huu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari
hizi, wasichana hao walioko kijijini kwao Ikonda, walisema masomo
waliyotofautiana katika ufaulu ni Kemia ambalo Maria amepata C na Consolata D
na Kiingereza ambalo Maria amepata B na Consolata B+.
Katika matokeo hayo ambayo kila mmoja
alikuwa na namba yake ya mtihani (Maria-S. 283/0004 na Consotala S 283/0009),
masomo ambayo wamelingana ni Uraia wakiwa na E, Historia C, Jiografia E,
Kiswahili C, Bayolojia B na Hesabu C.
“Tumefurahia sana kufaulu, tutaendelea
na masomo ya kidato cha tano na sita shuleni hapo Julai, tutasoma mchepuo wa
CBG (Kemia, Bayolojia na Jiografia) au HGL, (Historia, Jiografia na
Kiingereza),”
alisema Consolata.
Aliendelea kusema, “tunatarajia
kwenda Shule ya Sekondari ya Udzungwa iko karibu na shule tuliyosoma kidato cha
kwanza hadi cha nne ya Maria Consolata kule Kidabaga, Kilolo.”
Kwa upande wake Maria, alisema
amefurahi na matumaini yao ni kujitahidi kusoma kwa bidii zaidi wafaulu na
kujiunga na elimu ya juu.
“Nimefurahi mimi na Consolata,
tulipigiwa simu na walimu wakatuambia matokeo yetu, mama yetu mlezi amefurahi
na Mungu akipenda tutaanza masomo mwezi Julai; ya kidato cha tano,”alisema Maria ambaye
kwa mujibu wake, wana ndoto za kuwa wahasibu.
Alisema kwa sasa wako likizo
wamepumzika nyumbani kwao Ikonda chini ya uangalizi wa mama yao mlezi na dada
yao msaidizi, Magdalena Mbilinyi. Wanatarajia kurudi Kilolo, kwenye Kituo
cha Nyota ya Asubuhi kati ya Machi 7 na 14, mwaka huu.
Mama mlezi wao, Bestina Mbilinyi
alieleza furaha kwa ufaulu huo wa watoto wake.
“Nimefurahi sana, wanangu wamefaulu na
wataendelea na masomo ya Kidato cha Tano, hivi sasa wamekuja likizo kunisalimu,
ila wataondoka baada ya siku chache kurudi kituoni Nyota ya Asubuhi, huku
Kilolo,”
alisema Bestina.
Akizungumza na mwandishi, Mkuu wa Shule
ya Sekondari Maria Consolata, Jefred Kipingi, wamefurahia matokeo ya wasichana
hayo.
“Kwa kweli tumefurahi matokeo ya kina
Maria na Conso, wataenda kidato cha tano, ila kwa jinsi walivyo, watasoma hapa
hapa karibu ili iwe rahisi uangalizi wao, hivyo watasoma Shule ya Sekondari
Udzungwa, iko karibu na hapa wanapoishi,”alisema Kipingi.
Akizungumzia ufaulu kwa ujumla wa shule
hiyo waliyosoma pacha hao, Mkuu huyo wa shule alisema siyo mazuri kwa kutokana
na kuwapo wanafunzi wengi waliofeli mwaka huu.
“Kwa mwaka huu matokeo siyo mazuri ,
pacha hao ni kati ya wanafunzi wanane waliopata alama ya Credit, ila ufaulu kwa
ujumla siyo kama miaka iliyopita, tuliliona hili tangu mwanzo kutokana na aina
ya wanafunzi tuliokuwa nao kidato hicho,” alisema Mwalimu Kipingi.
Septemba 18, mwaka jana, mtandao
huu ulichapisha habari na picha ya pacha hao iliyozungumzia matarajio yao ya
kufanya mtihani wa kuhitimu Kidato cha Nne, Novemba mwaka jana.
Walihitimu Shule ya Msingi mwaka 2009,
kijijini kwao Ikonda, wakiwa na umri wa miaka 13. Walipangiwa kujiunga na
Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo hawakujiunga na sekondari
hiyo, kutokana na hali yao na pia umbali kutoka Iringa hadi Dar es Salaam.
Wamisionari Wakatoliki wa Italia wa Kituo cha Nyota ya Asubuhi kilichoko Kilolo, mkoani Iringa, waliwachukua mwaka 2011 na kuanza kidato cha kwanza katika shule yao ya Maria Consolata iliyoko Kidabaga, Kilolo.
Wamisionari Wakatoliki wa Italia wa Kituo cha Nyota ya Asubuhi kilichoko Kilolo, mkoani Iringa, waliwachukua mwaka 2011 na kuanza kidato cha kwanza katika shule yao ya Maria Consolata iliyoko Kidabaga, Kilolo.
Katika maisha yao ya kusoma, kila mmoja
alikuwa na madaftari yake na wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi
wanazopewa, mmoja huanza kuandika, akimaliza na mwingine huandika.
“Wala hatupati shida tumezoea, kila
mmoja anafanya kazi yake, mimi naandika kwa mkono wa kushoto na Maria anaandika
kwa mkono wa kulia,” anasema
Consolata, ambaye anaonekana kuwa mchangamfu zaidi.
Mabinti hao walizaliwa katika
Hospitali ya Misheni ya Ikonda mwaka 1996, wilayani Makete mkoani Njombe.
Taarifa zao hazikufahamika hadi
walipoandikishwa kuanza elimu ya msingi Ikonda na kutafutiwa mlezi wa
kuwaangalia, baada ya wazazi wao kufariki dunia wakiwa wadogo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAPACHA WA MAKETE WALIOUNGANA KUINGIA KIDATO CHA TANO.”
Post a Comment