Saturday, October 31, 2015
TAARIFA YA ZADIA KUHUSU KUFUTWA KWA MATOKEO YA UCHAGUZI ZANZIBAR.
Do you like this story?
Jumuiya ya Wazanzibari Waishio Nchini Marekani
(ZADIA), imekuwa ikifuatilia kwa karibu na makini zaidi zoezi zima la Uchaguzi
Mkuu visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Kwa kiasi kikubwa mchakato wa
uchaguzi ulifanyika kwa njia za amani na utulivu. Hata hivyo ZADIA imeshtushwa
mno na tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Mh. Jecha Salim
Jecha la kutangaza kuufuta Uchaguzi Mkuu Zanzibar na matokeo yake.
Ama kwa hakika kitendo hicho hakikuwa cha
busara na kinapelekea kurudisha nyuma maendeleao ya demokrasia Zanzibar, na
vilevile hakiashirii mustakbali mwema kwa nchi yetu tuipendayo. Wazanzibari
wameelezea maoni na matakwa yao kwenye visanduku vya kupigia kura, na maoni na
matakwa yao hayo yanapaswa kusikilizwa na kuheshimiwa.
Kwa hivyo, ZADIA inatoa wito kwa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi Zanzibar, kumalizia mchakato mzima wa kuhesabu kura kwa majimbo
yaliyobakia na kutoa matokeo ya mwisho ya Uchaguzi na kumtangaza mshindi ili
kuiepusha Zanzibar yetu tuipendayo kuingia katika hali ya mtafaruku na
mifarakano isiyokuwa na tija bali kuleta hasara.
ZADIA pia inaungana na jumuiya zote za
kimataifa ambazo zimetoa msimamo wao juu ya uchaguzi wa Zanzibar, hasa ubalozi
wa Marekani nchini Tanzania, ambao ni kiungo madhubuti kati ya Wazanzibari
walioko Zanzibar na wenzao wanaoishi nchini Marekani.
Aidha, tunapenda kumkumbusha Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Dakta Ali Mohammed Shein kuwa Wazanzibari walimpa amana kubwa ya
kuwaongoza, na kwa hivyo ni wajibu wake kuienzi amana hiyo kwa kuchukuwa hatua
za kiungwana za kuitoa Zanzibar kwenye mgando huu wa kisiasa. Hali hii iliyopo
sasa inaleta wasiwasi miongoni mwa raia na imekua ikiathiri maisha yao ya kila
siku, na ikiachwa kuendelea huenda ikaathiri pia mustakbali maisha yao kwa
jumla.
ZADIA pia inamtolea wito Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
kutumia mamlaka yake aliyonayo kuhakikisha Zanzibar inatoka kwenye mkwamo huu
wa kisiasa na kwamba anaondoka madarakani akiiacha Zanzibar ikiwa katika hali
ya amani na utulivu. Kwa kufanya hivyo atauthibitishia ulimwengu kuwa kweli
Tanzania ni kisima cha amani.
Na mwisho tunawaomba Wazanzibari, wapenzi wa
Zanzibar, na Watanzania wote kwa ujumla popote pale walipo, wajitahidi kufanya
mawasiliano na Jumuiya nyengine za Kimataifa ili ziingilie kati suala hili
kabla nchi yetu haijaingia kwenye mtafaruku mkubwa wa kisiasa na kijamii na
hata kupelekea kuhatarisha amani ya nchi yetu.
Mungu Ibariki, Zanzibar.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TAARIFA YA ZADIA KUHUSU KUFUTWA KWA MATOKEO YA UCHAGUZI ZANZIBAR.”
Post a Comment