Wednesday, January 27, 2016

BAADA YA KUZAWADIWA KIWANJA KIGAMBONI, WASANII WAMFANYIA SAMATTA BONGE LA SURPRISE




Na Mwandishi Wetu, Mkuranga
MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) umeamua kumpa uanachama wa heshima mchezaji bora wa Afrika, Mbwana Samatta pamoja na kumzawadia ekari tano za ardhi katika kijiji cha Wasanii Mwanzega, Mkuranga kwa ajili ya kuanzisha Chuo cha Mafunzo ya soka.

Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib alisema jana kuwa kikao cha Kamati ya Utendaji ya Mtandao huo kilichoketi juzi kilifikia uamuzi huo baada ya kufuatilia kwa karibu mafanikio ya Samatta akiwa na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kongo na kufanya vizuri katika mashindano ya Afrika hadi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora Afrika.

Alisema SHIWATA inatoa kiwanja hicho kama zawadi kwa mchezaji huyo kutokana na uwezo wake wa kulitangaza taifa katika medani ya kimataifa katika mchezo wa soka ambako wengine watafuata nyayo zake.

Taalib alisema taratibu za makabidhiano zinafanywa kwa mawasiliano na baba yake mzazi, Ali Samatta na atakabidhiwa eneo hilo mara baada ya kurudi kutoka Ubelgiji ambako anakwenda kusaini mkataba na timu ya KRC Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji wa miaka minne.

SHIWATA yenye wanachama zaidi ya 8,000 inamiliki ekari 300 za kujenga makazi, kumbi za starehe, viwanja vya michezo na nyumba za kuishi katika kijiji cha Mwanzega wilayani Mkuranga na ekari 500 eneo la Ngarambe kwa ajili ya kilimo.

Wakati huo huo wasanii wanne maarufu nchini wakiongozwa na Ahmed Olotu ‘Chilo’ juzi walinogesha tamasha la sanaa na michezo wilayani Mkuranga walipoalikwa kuona sanaa inavyochezwa na wasanii wa wilaya hiyo.

Mzee Chilo aliyefuatana na Boniface Mwanza Mpango ‘King Kikii’, Wasanii wa Bongo Movie, Suzan Lewis ‘Natasha, Kulwa Kikumba ‘Dude’ na Asha Salvador walijikuta wakishangiliwa mara kwa mara na wasanii wenyeji ambao pia walipiga nao picha.

0 Responses to “BAADA YA KUZAWADIWA KIWANJA KIGAMBONI, WASANII WAMFANYIA SAMATTA BONGE LA SURPRISE”

Post a Comment

More to Read