Monday, January 18, 2016
BOT YAIPIGA FAINI STANBIC SH BILLION TATU
Do you like this story?
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawamo pichani) jijini Dar es Salaam |
BENKI Kuu (BoT) imeitoza faini Benki ya
Stanbic Sh bilioni tatu baada ya kubaini benki hiyo imefanya miamala ya kutia
shaka inayohusu malipo kwa kampuni ya Kitanzania ya EGMA ya Dola za Marekani
mil.6 zilizoingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo na kutolewa ndani ya muda
mfupi.
Stanbic iliwezesha Serikali ya Tanzania kuuza
hati fungani za dola milioni 600 (Sh trilioni 1.3) kwa benki ya Standard
Chartered ya Uingereza. Mauzo hayo yalifanyika mwaka 2012 kwa Serikali kwa
masharti ya kulipwa riba ya asilimia 1.4; lakini Stanbic tawi la Tanzania
iliongeza asilimia moja na hivyo kufanya Serikali ya Tanzania kutakiwa kulipa
riba ya asilimia 2.4.
Adhabu iliyotangazwa jana na Serikali kwa
benki hiyo, inatokana na Stanbic kuilipa EGMA Dola za Marekani milioni 6 ambazo
ziliingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo ya kitanzania na kutolewa kwa muda
mfupi kwa njia ya fedha taslimu, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za
kibenki.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha
na Mipango, Dk Philipo Mpango alisema BoT katika uchunguzi wake, imebaini
malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za
kibenki na yalihusisha uongozi wa Benki ya Stanbic.
Dk Mpango alisema BoT imechukua hatua ya
kutoza faini benki hiyo kama onyo iweze kuwa makini katika kuhakikisha shughuli
zake zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kibenki za kuzingatia sheria.
“Hatua hii ni onyo kwa benki na taasisi
zingine za fedha zisijihusishe na makosa ya aina hiyo ambayo ni kinyume cha
taratibu za kibenki na uvunjaji wa sheria za nchi,” alisema Dk Mpango.
Waziri alifafanua kuwa sheria inaitaka Benki
ya Stanbic kutoa utetezi katika siku 20 ambazo zitaisha Januari 30 mwaka huu.
“Endapo BoT haitaridhika na utetezi wake,
Benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo,” alisema.
Alisema hatua kali zitaendelea kuchukuliwa
kwa benki au taasisi ya fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu
za kibenki na sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Uchunguzi wa BoT
Akielezea hatua za uchunguzi huo, Dk Mpango
alisema taarifa ya uchunguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu
wa taratibu na BoT iliagiza bodi ya wakurugenzi ya benki kuchukua hatua stahiki
za kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Alisema benki hiyo pia iliagizwa kutoa
taarifa kwa kitengo kinachochunguza makosa ya fedha (FIU) kilichoko Wizara ya
Fedha na Mipango kuhusu miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA kama
sheria ya kuzuia utakatishaji wa fedha haramu inavyoelekeza.
“Benki ya Stanbic ilitekeleza maagizo na
kutoa taarifa FIU kuhusu miamala hiyo iliyotiliwa shaka,” alisema Dk Mpango.
Dk Mpango alisema ripoti hiyo ya BoT pia
iliombwa kutumiwa na Shirika la Upelelezi la Makosa Makubwa (SFO) katika kesi
dhidi ya Benki ya Standard ambayo waliruhusu itumiwe kwa kuzingatia chanzo cha
ripoti hiyo.
“Hatimaye Standard ilikubali makosa na
ilitozwa faini ya jumla ya dola za Marekani milioni 32.20 na kiasi cha dola za
Marekani milioni saba zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania,” alisema Dk Mpango na
kufafanua kuwa dola milioni 6 zilikuwa ni fidia na dola milioni moja ni riba.
Takukuru yawahoji
Akijibu maswali ya waandishi wa habari ambao
walitaka kufahamu wahusika wengine wamechukuliwa hatua gani, Dk Mpango alisema
bado Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inaendelea na
uchunguzi katika makosa yanayohusu rushwa.
“Hili ambalo limefanyika leo ni kuhusu
uchuguzi wa BoT kuhusu masuala ya miamala ya kifedha, sasa kuna vyombo vingine
vya dola vinaendelea kuwahoji wahusika na wakikamilisha kazi yao watatangaza
hatua za kuchukua,” alisema Dk Mpango.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BOT YAIPIGA FAINI STANBIC SH BILLION TATU”
Post a Comment