Monday, January 18, 2016

GOLI LA ROONEY DHIDI YA LIVERPOOL LAWEKA REKODI EPL





Nahodha na mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney jana aliingia katika vitabu vya historia mara baada ya kuifungia timu yake goli la ushindi dhidi ya mahasimu wao Liverpool katika mchezo wa ligi kuu nchini England.

Goli hilo la Rooney lilikua ni la 176 kwake akiifungia timu moja (Manchester United) na kumuacha mkongwe Thierry Henry katika nafasi ya pili kwa magoli 175 yote aliyafunga akiwa Arsenal, huku kinara wa mabao wa muda wote katika historia ya ligi kuu nchini England Alan Shearer akibakia katika nafasi ya tatu na magoli 148 aliyoifungia Newcastle United pekee.

Rooney ameendelea kujiweka katika wakati mzuri na kulifanya jina lake lidumu katika vitabu hata atakapotundika daluga kutokana na kuendelea kuvunja na kuandika rekodi zake mwenyewe, ambapo hadi sasa amekwisha vunja rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya England huku pia akikaribia kuivunja rekodi inayoshikiliwa na Sir Bob Chalton ya ufungaji bora wa klabu ya Manchester United.

Aidha katika mchezo wa jana dhidi ya Liverpool, Wayne Rooney alifunga goli hilo la ushindi katika dakika ya 78 na kuwa ni goli lake la ushindi kwa United dhidi ya Liverpool tangu alipofanya hivyo miaka 11 iliyopita mwaka 2005 katika uwanja wa Anfield.

Fomu ya Rooney imeendelea kuimarika tangu kuanza kwa mwaka huu mpya wa 2016 kwani sasa amefunga magoli 5 kati ya michezo 4 mfululizo na kuisaidia klabu yake ya United kurudi katika mstari mara baada ya kutetereka miezi michache iliyopita.

0 Responses to “GOLI LA ROONEY DHIDI YA LIVERPOOL LAWEKA REKODI EPL”

Post a Comment

More to Read